Baraza lanusa ufisadi kilimo pilipili kichaa

15Feb 2020
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Baraza lanusa ufisadi kilimo pilipili kichaa

BAADHI ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wameitaka Mamlaka ya Kupambana na Rushwa (ZAECA) kufanya uchunguzi wa ufisadi kwenye mradi wa kilimo cha pilipili kichaa.

Walitaka hatua ichukuliwe kwani mradi huo umetengewa takribani Sh. milioni 500 lakini hadi sasa hakuna kilichofanyika katika mchanganuo wa fedha hizo na matumizi yake.

Akizungumza katika Baraza la Wawakilishi, Mwakilishi wa jimbo la Uzini Mohamed Raza, alisema serikali malengo yake ni mazuri ya kupambana na tatizo la ajira kwa vijana na kuamua kutenga fedha milioni 500 kwa ajili ya kujiajiri na kazi za ujasiriamali.

Hata hivyo, alisema utekelezaji wa mradi huo umeingia katika utata mkubwa ambapo hadi sasa hakuna hata eka moja ya kilimo cha pilipili iliyovunwa katika mashamba yaliyotengwa ikiwamo Bambi na Pangatupu.

''Jamani Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mnamwangusha sana Rais Shein ambaye lengo lake la kuwawezesha vijana kujiajiri halijatamia.....mradi huu umetengewa fedha nyingi lakini huu ni mwezi wa sita hakuna kilichofanyika''alisema.

Mwakilishi wa jimbo la Bumbwini Mtumwa Peya, aliitaka wizara kabla ya kutekeleza mradi kufanya utafiti wa kina na kujua maeneo yepi ni muafaka kwa ajili ya kuendeleza kilimo cha pilipili hoho.

Peya alisikitishwa na fedha zilizotengwa kwa vijana katika mradi wa pilipili hoho kuwa ni sawa na zilizopotea kwa sababu hakuna mafanikio ya kilimo hicho ambapo vijana hawakupata mashirikiano kutoka kwa wataalamu.

Alieleza kuwa katika eneo hilo mradi ambao unakubali ni wa kuotesha miwa ambao unatekelezwa na vikundi mbali mbali vya wajasiriamali huku ukipata mafanikio makubwa.

''Wananchi wangu wa Pangatupu kwa muda mrefu wamekuwa wakitekeleza mradi wa kuotesha miwa ambao umeleta mafanikio makubwa na sio huu mradi wa Pilipili hoho''alisema.

Kwa upande wake mwakilishi wa viti maalumu wanawake Vijana Salma Mohamed Mwinjuma aliitaka wizara kukaa pamoja na vijana kuweka mikakati ambayo itawawezesha kuimarisha kilimo hicho kwa mafanikio makubwa.

''Vijana wetu wapo tayari kushiriki kikamilifu katika kilimo cha pilipili hoho ambacho kimeonyesha mafanikio makubwa''alisema.

Awali akizungumza kuhusu sakata la mradi huo, Waziri wa Biashara na Viwanda Balozi Amina Salum Ali, alisema vijana walioteuliwa kushiriki katika mradi huo hawakuonesha mashirikiano na utayari wa kutekeleza mradi huo.

''Vijana tuliowachaguwa kushiriki katika mradi wa pilipili hoho hawakuonyesha utayari na mashirikiano mazuri ya kufanya kazi hizo na ndiyo maana mradi umeyumba''alisema.

Habari Kubwa