Baraza lataka utalii kwa wote

09Nov 2019
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Baraza lataka utalii kwa wote

KAMATI ya Kudumu ya Habari na Utalii ya Baraza la Wawakilishi , imeitaka Kamisheni ya Utalii kuzipatia elimu ya kutosha kamati za wilaya za utalii ili kufikia dhana nzima ya utalii kwa wote.

Akizungumza na Kamati za Wilaya za Utalii huko katika Ukumbi wa Wizara ya Habari Utalii na Mambo ya Kale Mjini Zanzibar Mwenyekiti wa kamati hiyo Mwantatu Mbaraka Khamis, alisema kamati hizo zikipatiwa elimu ya kutosha zitaweza kufanyakazi kwa ufanisi na kutekeleza vyema majukumu yao.

Alisema kumekuwa na changomoto mbalimbalii zinazoikumba dhana nzima ya utalii kwa wote hivyo ni vyema kamati hizo kupatiwa mafunzo na kuelimisha jamii ili kufikia lengo lililokusudiwa.

“Fursa hii ya elimu itaufanya utalii kwa wote kufaidisha wananchi wazawa kwani kamati zitaweza kufanya kazi kwa weledi na kutatua changamoto zilizopo”,alieleza mwenyekiti huyo.

Kwa upande wao wajumbe wa kamati za wilaya walisema zitafanya kazi kwa kuangalia maslahi ya Wazanzibari na serikali kwa ujumla ili kufikia dhana ya utalii kwa wote na si kuwanufaisha zaidi wageni na kuwasahau wazawa.

Aidha, waliomba kupatiwa ushirikiano na taasisi nyingine pamoja na wananchi ili kudhibiti biashara haramu katika fukwe, kulinda Mila, silka na Utamaduni wa Mzanzibari pamoja na maeneo ya kihistoria yasiharibiwe kwa lengo la kuongeza pato nchini.

Mapema Katibu Mtendaji Kamisheni ya Utalii Abdallah Muhamed Juma, alisema kamati za kiwilaya zitashirikiana na kamisheni kwa ajili ya kusukuma mbele maendeleo ya utalii ndani ya wilaya.

Aidha, Katibu Mtendaji alisema kamati hizo zitakuwa na majukumu ya kuimarisha utalii kwa wote, kudhibiti usalama na amani kwa wageni na wenyeji wa maeneo ya utalii, kuazisha mfumo wa fedha wa jamii kwa kutoa asilimia moja ya pato la muekezaji ambazo zitatumika kwa maendeleo ya vijiji.

Alisema pia kamati hizo zitakuwa na jukumu la kulinda na kudumisha utamaduni za asili kama bidhaa ya utalii, kudhibiti thamani, maadili katika wilaya kudhibiti pamoja na kuunga mkono jumuiya za kiraia zinazofanya shughuli za utalii kwa kuzisaidia kwa kujishuhulisha katika mipango yao kwa kushirikiana na kamisheni na wadau wengine wa utalii.

Habari Kubwa