Bei ya saruji kushuka

21Aug 2018
Elizaberth Zaya
DAR ES SALAAM
Nipashe
Bei ya saruji kushuka

BEI ya saruji inatarajiwa kushuka nchini kutokana na Shirika la Taifa la Maendeleo ya Petroli (TPDC) kuingia mkataba wa kuiuzia gesi asilia kampuni ya kutengeneza saruji ya Dangote - Tanzania.

Mkataba huo uliosainiwa jijini Dar es Salaam jana, utasaidia kiwanda hicho ambacho kilikuwa kimesitisha uzalishaji, kuachana na matumizi ya mafuta ya dizeli katika uzalishaji wa umeme na kutumia gesi hiyo. 

Ilielezwa jana kuwa makubaliano baina ya pande hizo mbili, sasa yanatarajia kukiwezesha kiwanda hicho kuongeza kiwango cha uzalishaji wa umeme kutoka wastani wa MW 20 (18MW-22MW) hadi MW 35. 

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kiwanda cha Dangote, Jagat Rathee, alisema jana kuwa kabla ya kuanza kutumia gesi hiyo, kiwanda hicho kilikuwa kinatumia wastani wa lita 106,000 za dizeli kwa siku katika uzalishaji wa tani 2,000 za saruji. 

Rattee alisema makubaliano hayo yamekuja kwa wakati mwafaka na yatasaidia kiwanda hicho kuongeza kiwango cha uzalishaji wa saruji kutoka wastani wa tani 2,000 hadi 6,000 kwa siku kutokana na kushuka kwa gharama za uzalishaji. 

Rattee pia alisema kiwanda hicho kitaanza kutumia rasmi umeme huo wa gesi asilia ndani ya siku 30 zijazo kuanzia jana. 

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Kapuulya Musomba, alisema mkataba huo utadumu kwa miaka 20. 

Alisema kiwanda hicho ni sehemu ya viwanda saba vilivyopo kwenye mpango wa shirika hilo kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2018/19 na kwamba viwanda vingine sita vinatarajiwa kuunganishwa siku za usoni. 

”Tunafahamu kwamba serikali iko katika hatua za kujenga uchumi wa viwanda, hivyo sisi (TPDC) kwa nafasi yetu tumejipanga kuhakikisha viwanda vinazalisha bidhaa kwa gharama nafuu kupitia matumizi ya gesi asilia,” alisema na kuongeza: 

”Tunatarajia wataanza kutumia futi za ujazo milioni nane na baada ya miaka miwili ijayo, wataanza kutumia futi za ujazo milioni 20.” 

Kiwanda cha Dangote sasa kinakuwa miongoni mwa viwanda 42 vinavyotumia gesi asilia katika kuzalisha umeme unaofikia futi za ujazo milioni 15 kutoka katika akiba ya futi za ujazo trilioni 57 zenye uwezo wa kutumika miaka 40 ijayo. 

Kusitisha uzalishaji kwa kiwanda hicho kutokana na changamoto ya nishati kumeifanya bei ya saruji kupanda kwa kasi kutoka wastani wa Sh. 12,500 Januari mwaka huu hadi Sh. 18,000 huku visiwani Zanzibar ikiuzwa Sh. 24,000 kwa mfuko wa Kg 50.

Habari Kubwa