Benki Kuu yaiganda FBME

22Sep 2016
Gwamaka Alipipi
Nipashe
Benki Kuu yaiganda FBME

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema benki ya FBME bado inaendesha shughuli za kibenki chini ya usimamizi wako, licha ya notisi ya kuifunga iliyotolewa Julai 15, 2014 na Taasisi ya Marekani inayopambana na utakatishaji wa fedha kupitia mtandao (FinCEN).

FinCEN katika notisi yake hiyo ilitoa kusudio la kuifungia FBME kutotumia mfumo wa kibenki wa Marekani.
Baada ya notisi hiyo, FinCEN na FBME wamekuwa katika mashauriano baada ya uamuzi wa Mahakama ya Marekani iliyoitaka FinCEN irudie mchakato mzima uliotumika kabla ya kufikia uamuzi wa mwisho.

Kadhalika, Machi 25, mwaka huu, FinCEN ilitoa uamuzi wa mwisho ambao ulizitaka benki na taasisi za fedha za Marekani kutofungua akaunti na kutojihusisha kibiashara na FBME.

Alipoulizwa na Nipashe jana kuhusu hatua ambazo BoT imeshaichukulia FBME baada ya kushtumiwa na FinCEN kujihusisha na biashara ya utakatishaji wa fedha haramu na hatua ya Benki Kuu ya Cyprus kuliweka tawi la FBME lililoko nchini humo chini ya uangalizi maalumu, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Benki wa BoT, Kennedy Nyoni, alisema shughuli za kibenki za FBME bado zipo chini ya usimamizi wa BoT.

"Ninachoweza kukisema ni kuwa bado ipo chini ya uangalizi maalum wa BoT, na bado inafanya kazi hapa nchini japokuwa nchi zingine zimezuiliwa," alisema Nyoni.

Mei 4, mwaka huu, gazeti hili ilipokea taarifa kutoka kitengo cha mawasiliano cha BoT kuhusu FBME ambayo ilieleza kuwa BoT imeiweka benki chini ya usimamizi maalumu tangu Julai 24, 2014.

"Kwa kuzingatia uamuzi wa mwisho wa FinCEN, ambao utakuwa rasmi siku 120 baada ya kuchapichwa katika Sajili ya Shirikisho ya Marekani, na matakwa ya sheria nchini Tanzania, Benki Kuu inakamilisha mapitio ya hali ya sasa ya FBME ambayo itapelekea kuchukua hatua stahiki za kuhitimisha suala hili,” ilieleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa uamuzi huo wa mwisho wa FinCEN utaathiri kwa kiwango kikubwa uendeshaji mzima wa FBME kwa kuwa benki hiyo haitaweza tena kufanya miamala ya kimataifa na kupata huduma za mifumo ya kibenki na hivyo itashindwa kutoa baadhi ya huduma muhimu kwa wateja wake.

Habari Kubwa