Benki ya Dunia yajitosa ujenzi reli, umeme Rufiji

22Apr 2018
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe Jumapili
Benki ya Dunia yajitosa ujenzi reli, umeme Rufiji

BENKI ya Dunia imeonesha nia ya kuisaidia Tanzania katika ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa (SGR), kutoka Isaka kwenda Rusumo na baadaye Kigali nchini Rwanda.

RELI.

Sambamba na reli hiyo, benki hiyo pia inakusudia kusaidia mradi wa umeme katika Mto Rufiji na ujenzi wa miundombinu mingine ya usafirishaji  kama barabara ili kusaidia kuendeleza biashara na ustawi wa jamii kwa ujumla.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alisema hayo juzi wakati wa majadiliano na wataalamu wa Benki ya Dunia yaliyoongozwa na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayeshughulikia kanda ya Afrika, Makhtar Diop, kwenye mikutano ya mwaka ya kipupwe inayoendelea Washington DC, Marekani.

Dkt. Mpango alisema miradi ya kikanda ambayo benki hiyo imeonyesha nia ya kuitekeleza ni ile ya uboreshaji wa mazingira na bandari katika Ziwa Victoria zikiwamo za mikoa ya Mwanza, Musoma na bandari zilizoko katika Ziwa Tanganyika ambazo zitarahisisha usafiri wa kwenda Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

‘Miradi hii ya kikanda na kitaifa ambayo Benki ya Dunia imepanga kuitekeleza kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania kwa mwaka ujao wa fedha, itahakikisha kunakuwa na mazingira endelevu na tija kwa kuwa inagusa nchi zote zinazozunguka maziwa hayo mawili,” alisema. 

Alisema ni lazima kuhakikisha kunakuwa na udhibiti wa uchafuzi wa mazingira kadri iwezekanavyo ili kuendelea kufaidi rasilimali za maziwa hayo makubwa  kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania na nchi jirani zinazozunguka maziwa hayo.

Pia alisema kwa mwakani, Benki ya Dunia imeonyesha nia ya kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kuzalisha umeme katika Mto Rufiji eneo la Ruhuji ambao pindi utakapokamilika unatarajiwa kuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 300.

‘Eneo hili la sekta ya umeme ni muhimu sana kwa ajili ya maendeleo ya viwanda kwa kuwa uchumi wa viwanda hauwezi kukua bila kuwapo umeme wa uhakika’ alifafanua Waziri Mpango.

Katika hatua nyingine, Benki ya Dunia imekubali kuisaidia Tanzania kutoa mafunzo katika uchambuzi wa miradi mbalimbali ili kusadia kutoingia kwenye madeni makubwa zaidi ambayo hayawezi kulipika.

Waziri Mpango alisema  kutokuwa na ufanisi wa kutosha katika kuchambua miradi ambayo inagharamiwa na fedha za mikopo, kunasababisha nchi kubeba mzigo mkubwa wa madeni, hivyo ni vyema Tanzania ikahakikisha kuwa miradi hasa ile inayogharamiwa kwa fedha za mikopo inachambuliwa vizuri ili mradi husika unapokamilika uweze kulipa deni.

Alisema kwa mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali itakuwa na miradi mingi ya kutekeleza, ikiwamo ya kupambana na utapiamlo, hivyo ni vyema nchi ikaangalia namna bora ambayo Benki ya Dunia inaweza kusaidia.

“Kitaalamu mpaka mwanadamu anapofikisha siku 1,000 ni kipindi muhimu sana kinachoamua maisha yake atakapokuwa mtu mzima atakuwa na uwezo gani wa kufikiri.  Kutokana na hali hiyo mtu ambaye atakuwa na utapiamlo uwezo wake utakuwa mdogo zaidi kulinganisha na mtoto aliyepata lishe bora,” alisema. 

Mikutano ya mwaka ya majira ya kipupwe, kati ya ujumbe wa serikali ya Tanzania na wataalamu wa Benki ya Dunia imekuwa na mafanikio makubwa kwa kuwa Tanzania itanufaika kutokana programu mbalimbali ambazo zitagharamiwa na benki hiyo kwa mikopo nafuu. 

Habari Kubwa