Benki ya NMB yamwaga vifaa vya shule vya mil. 20/-

07Dec 2018
Cynthia Mwilolezi
Arusha
Nipashe
Benki ya NMB yamwaga vifaa vya shule vya mil. 20/-

BENKI ya NMB imetoa msaada wa vifaa mbalimbali kusaidia shule katika Wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha, vyenye thamani ya Sh. milioni 20.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Kaimu Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Kaskazini, Cosmas Gabrieli, alisema benki hiyo itambua juhudi za serikali kwa kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bure kuanzia shule ya msingi mpaka kidato cha nne.

Alisema kufuatia hali hiyo, benki hiyo imeona ni vyema ikaungana na serikali kwa kuunga mkono sekta ya elimu kwa kutoa msaada wa mabati 166, meza 166 za maabara, madawati 62 pamoja meza 62.

Aliongeza kuwa benki hiyo imekuwa ikipokea maombi mengi ya kuombwa msaada, lakini imejikita kusaidia sekta ya elimu, afya na majanga yanayopata waathirika kwa kuwa maeneo hayo, yanawagusa wananchi wanyonge wasiokuwa na uwezo.

Wakizungumza baada ya Mkuu wa Wilaya hiyo, kupokea msaada huo, wananchi waliohudhuria katika hafla hiyo walisema benki hiyo imekuwa ikichochea maendeleo hususani sekta ya elimu.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Lomunyaki Mollel, alisema msaada huo umekuwa faraja kubwa kwao, kwa kuwa watoto wao watakuwa na uhakika wa kuanza masomo mwezi Januari.

“Tunaishukuru Benki ya NMB kwa msaada huu mkubwa kwa kuwa watoto wetu walikuwa wanalazimika kutembea umbali mrefu na wakati mwingine wanafunzi wa kike walikuwa wanarubuniwa kwa kupewa lifti na madereva bodaboda, hali iliyokuwa inawasababishia kupata ujauzito na kuacha masomo,”alisema.

Habari Kubwa