Benki yaondoa tozo dola

22Oct 2018
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Benki yaondoa tozo dola

INTERNATIONAL Commercial Bank (ICB) imeondoa tozo kwa wateja wanaoweka dola za Marekani katika benki hiyo kama moja ya vivutio katika

Ushindani wa soko huria, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Ramakrishna Marakani, alisema jijini Dar es Salaam jana, kuwa pia benki yake itatoza kiwango sawa wakati wa kuhamisha fedha kutoka benki yao kwenda benki nyingine kama sehemu ya kuimarisha huduma zake kwa wateja.

Alisema mabadiliko hayo yana lengo la kuvutia wateja wengi zaidi na kujiweka katika nafasi nzuri ya ushindani wa soko na kwamba mabadiliko hayo pia ni motisha kwa wateja.

“Tumepunguza riba ya mikopo kwa wateja wetu, tutaondoa tozo kwa wateja wa akaunti za amana na hundi kwa wateja wetu wanaochukua dola za Marekani. Kwa hiyo katika miezi michache ijayo tunatarajia mabadiliko haya yatavutia wateja wengi zaidi,” ameeleza Marakani.

Alisema wateja ni watu ambao hupenda na hustahili motisha na vivutio mbalimbali na kwamba hilo ndilo jambo ambalo benki yake imelifanya.

Alisema wito wa Rais John Magufuli wa kuzitaka benki kushusha riba juu ya mikopo na kuondoa tozo nyingine ili Watanzania wanufaike na kuwapo kwenye mabenki nchini ni tukio chanya nchini na kueleza kwamba benki yake tayari imekwisha punguza riba juu ya mikopo na kuwa inatoza kati ya asilimia 16 na 18 kulingana na aina ya mkopo. Hata hivyo, hakueleza kiasi kilichopunguzwa.

Marakani alisema wanajiandaa kidijitali na kuboresha mifumo yao ya kiteknolojia ili benki yao itoe huduma maridhawa kulingana na teknolojia inavyokuwa.

Ameongeza benki hiyo inawalenga wateja wenye umri wa kati ya miaka 18 na 25. “Wateja wa aina hii ndiyo watakaokuwa na uhusiana na benki yetu kwa muda mrefu ujao,” alidokeza kuwa hiyo ni mbinu ya benki yao katika kutafuta wateja wapya.

Mkuu wa Operesheni wa Benki hiyo, Christome Tembo, alisema “Hatua hizi tunazozichukua zina maana kubwa kwa wateja wetu.
Tumejipanga kuwa sehemu ya kichocheo cha maendeleo yao.”

Alisema ICB inaunga mkono jitihada zote za serikali ya kuleta mageuzi ya kiuchumi na hasa kujenga uchumi wa kati na viwanda ifikapo mwaka 2018.

Habari Kubwa