Meneja Mawasiliano wa TPB, Noves Moses, alisema hayo wakati akizungumza katika hafla ya kumtangaza Mohamed Issa Sipe (29), mkazi wa Usa River, kuwa mshindi wa simu ya mkononi, katika shindano la kuweka na kutoa pesa, kupitia huduma ya Western Union, linaloendeshwa na benki hiyo nchi nzima.
Alisema, benki hiyo, inatenga fungu maalumu kusaidia jamii zenye uhitaji katika maeneo ambayo inatoa huduma zake, kama sehemu ya kurudisha faida waliyoipata kwa jamii.
Alisema fedha hizo zimetumika kusaidia shughuli za maendeleo katika matawi mbalimbali nchini kama vile ujenzi wa madarasa, zahanati, ununuzi wa madawati, ujenzi wa matundu ya vyoo, mashuka na vitanda katika hospitali mbalimbali.
"Kwa kipindi cha mwaka ujao tumetenga Sh. milioni 200 kusaidia shughuli za kijamii katika maeneo yetu ambayo hadi sasa tuna matawi makubwa 30 na madogo 36 nchi nzima," alisema.
Meneja tawi la Usa River, Speratus Kamala, akizungumzia shindano hilo, alisema limeanza Oktoba mwaka huu na washindi waliopatikana katika droo ya kwanza ya promosheni ya Western Union iliyofanyika Novemba 16, walipatikana washindi saba, kati yao watano wa simu za mkononi na wawili kompyuta mpakato.Alisema lengo la kuanzisha shindano hilo ni kurudisha faida wanayoipata kwa jamii wanayohudumia, alitoa wito kwa wananchi kujitokeza katika kushiriki shindano hilo na kuweza kujipatia zawadi ya simu, kompyuta na fedha.
Alisema benki hiyo inatoa huduma mbalimbali ikiwamo mikopo kwa wastaafu, wafanyabiashara wadogo na wakubwa, vikundi mbalimbali pamoja na mikopo kwa ajili ya elimu na watu binafsi.
Mshindi wa shindano hilo, Sipe, mkazi wa Usa River alisema kushinda zawadi hiyo kumetokana na kuwa mtumiaji wa muda mrefu wa huduma ya Western Union katika kutuma na kupokea fedha.