Benki zaombwa kupunguzia riba wakulima

26Jul 2021
Renatha Msungu
Dodoma
Nipashe
Benki zaombwa kupunguzia riba wakulima

WAZIRI wa Kilimo, Prof. Aldolf Mkenda, ameziomba benki kupunguza riba ya mikopo kwa wakulima ili kuongeza uzalishaji kwenye kilimo cha alizeti.

Prof. Mkenda alitoa kauli hiyo juzi alipokuwa akifunga Wiki ya PASS Trust jijini Dodoma na kuzinduliwa kwa Kampuni ya Leasing ya kukopesha wakulima zana za kilimo bila dhamana na kwa riba nafuu.
 
Alisema serikali inatumia fedha nyingi kwa ajili ya kuagiza mafuta ya kula nje, hivyo kama wakulima watawezeshwa itasaidia kuongeza uzalishaji wa alizeti na kutosheleza kwenye viwanda.
 
“Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kwa ajili ya kuagiza mafuta na hii inatokana na viwanda vya alizeti kushindwa kuzalisha mbegu za mafuta kwa wingi ambazo zitasaidia viwanda hivyo kufanya kazi kwa mwaka mzima,” alisema Prof. Mkenda.


Aidha, alisema wizara itahakikisha wanapata mbegu bora ambazo wakulima wanaolima kwa mkataba
watapatiwa ili kulima zao hilo kwa wingi.

Pia alisema wizara hiyo imeanzisha operesheni ya miaka mitatu hadi minne yenye mikakati inayotekelezeka kwa ajili ya kukuza kilimo
cha alizeti.

“Tumeteua mikoa mitatu ambayo itapewa kipaumbele katika huduma za ugani ili kuwa mstari wa mbele kuzalisha zao la alizeti,” alisema.
 
Alizipongeza Sweden na Denmark kwa kujitokeza kusaidia juhudi za PASS TRUST kuhakikisha inakuwa imara ili kuendelea kutoa mikopo kwa wakulima.

“Nitajipanga kuwaona mabalozi wa nchi hizo ili fedha watakazotoa ziendelea kutumika kwa ajili ya manufaa,” alisema Prof. Mkenda.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya PASS TRUST, Anna Shanalingigwa, alisema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na wizara hiyo kwa ajili ya kuinua sekta hiyo nchini kwa kuwa asilimia 60 ya Watanzania wanategemea kilimo.

Shanalingigwa alisema PASS Trust ipo mstari wa mbele kuhakikisha wakulima wananufaika na fursa za mikopo ambazo zinatolewa na taasisi hiyo ili kujiinua kiuchumi.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka, aliwataka wakulima kuendelea kufanya kazi na PASS Trust kwa sababu itawasaidia kuwainua kiuchumi kutokana na mikopo ambayo wanatoa kwa wakulima.

Aliwashauri kujipanga kuanzisha mashamba ya zabibu na alizeti kwa kuwa ni mazao yanayostawi latika Mkoa huo na yana manufaa ya kibiashara.