Benki zatakiwa kwenda vijijini

26Jan 2021
Said Hamdani
Lindi
Nipashe
Benki zatakiwa kwenda vijijini

BENKI zinazohudumu mkoani Lindi, zimeshauriwa kuwa na utaratibu wa kutembelea wakulima vijijini kwa ajili ya kuwapa elimu ikiwamo ya ujasiriamali.

Lengo ni kuwafanya wawe na uelewa mkunwa  utakaowasaidia kujitokeza kwa wingi kuhifadhi na kuomba mikopo kwa ajili ya kuendeleza kilimo.

Ushauri huo umelilewa na wakulima wanachama wa Chama cha Ushirika cha Msingi (KITUMIKI AMCOS) cha Manispaa ya Lindi, wakati wa mkutano mkuu wa uchaguzi.

Wakulima hao kutoka maeneo ya Kitumbikwera, Kineng’ene, Tulieni na Mitwero, walishauri hayo kufuatia wataalamu wa Benki za CRDB, NMB na NBC kuudhuria mkutano huo kuwapa elimu ya umuhimu wa kutumia taasisi hizo kuweka fedha na kuomba mikopo kwa ajili ya kuendeleza kilimo.

Said Rashidi, Selemani Daudi (Mkilwa) na Bakari Rashidi walisema kushindwa kwa wakulima walio wengi kuacha kutumia Benki kuhifadhi fedha zao zinazotokana na mauzo ya mazao yao, kunachangiwa zaidi na kutokuwa na elimu ya kutosha kufahamu umuhimu wake.

Walisema kama kila mmoja atakuwa na uwelewa wa kutosha, utunzaji wa fedha na upatikanaji mikopo inayotolewa na mabenki inapatikana kwa wakati, wakulima wengi watajitokeza na kuwa mstari wa mbele katika kutumia taasisi hizo za kifedha, ikiwemo kuomba mikopo kuendeleza kilimo chao.

Aidha, wajumbe wa Mkutano Mkuu wa KITUMIKI AMCOs wamewashauri wataalamu wa benki zinazohudumu mkoani Lindi kutoendelea kubaki ofisini, badala yake wajitoe kufuata wateja (wakulima) wanaowahitaji kwenye maeneo yao na kuwapa elimu ya ufahamu.

Rashidi alisema wakulima wanasita kujitokeza kuomba mikopo wakihofia kupoteza mali zao  walizozitafuta kwa shida pale watakaposhindwa kurejesha mikopo waliyochukua kwa wakati unaohitajika.

Mkilwa aliwashauri watendaji wa benki kuharakisha utoaji wa mikopo  kwa wakulima wanaojitokeza kuomba ili waweze kuwahi shughuli zao za kilimo badala ya kusubiri kwa muda mrefu.

Wakijibu hoja za wanachama hao, watendaji wa benki hizo, Samuel Sunza (CRDB), Ndaki Madata (NMB) na Jovin Mapunda (NBC) walikiri kuwapo kwa upungufu huo, huku wakiahidi kuyafanyia kazi.

Habari Kubwa