Bidhaa za ndani zapigiwa debe

08Dec 2021
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Bidhaa za ndani zapigiwa debe

WATANZANIA wametakiwa kujenga utamaduni wa kuthamini bidhaa zinazozalishwa nchini ili kuwapa nguvu wawekezaji wa ndani katika kuzalisha na kuinua sekta ya viwanda.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdull, alisema hayo jana wakati wa ufunguzi wa maonyesho ya sita ya bidhaa za viwanda uliofanyika katika viwanja vya Maisara, mjini hapa.

Alisema Tanzania ina kila aina ya bidhaa zenye sifa na ubora, hivyo katika kuunga mkono jitihada za wazalishaji, hakuna budi kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini.

Hemed aliwataka washiriki wa maonyesho hayo kushiriki katika matukio mbalimbali ikiwamo mikutano ya kibiashara na kongamano la viwanda. Alisema kufanya hivyo kutawasaidia kujifunza, kubadilishana uzoefu na kukutana na wanunuzi wa bidhaa wanazozalisha.

Alisema Serikali ya Muungano na ya Zanzibar ziko katika mchakato wa kuimarisha mazingira mazuri ya viwanda kwa lengo la kuhimili ushindani wa masoko kwa kuwa na bidhaa bora zenye viwango.

Katika kuhakikisha lengo hilo linafanikiwa, alisema serikali ya Zanzibar imetenga Sh. bilioni 84.5 kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali kuimarisha biashara zao.

“Na kwa vile serikali imejikita katika kuendeleza uchumi wa buluu, kati ya fedha hizo, Sh. bilioni 36.5 zitaelekezwa katika sekta ya uvuvi na mazao ya baharini hususani mwani na dagaa,” alisema.

Hemed alisema serikali inaendelea na ukamilishaji wa ujenzi wa kiwanda cha mwani Pemba ambacho kitasaidia kuongeza thamani ya zao hilo na pato la wananchi.

Naye Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Omar Said Shaaban, alisema tangu kuasisiwa kwa maonyesho hayo mwaka 2016, wenye viwanda 500 wameshiriki na kwa mwaka huu wameshiriki 113 vikiwamo viwanda 10 vya Zanzibar na 23 kutoka Tanzania Bara.

Kauli mbiu ya maonyesho hayo ni “Tumia Bidhaa za Tanzania, Jenga Tanzania”.

Habari Kubwa