Bili maji Zanzibar kulipwa kidijitali

29Sep 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Bili maji Zanzibar kulipwa kidijitali

WATEJA wa Zantel sasa wanaweza kulipia bili za maji kiurahisi zaidi kwa njia ya Ezypesa baada ya kampuni hiyo kuingia ubia na Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA), mfumo wa kidigitali zaidi wa kufanya malipo.

Hatua hiyo itaongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato huku ikiwapunguzia wateja, adha ya kusafiri umbali mrefu, ili kulipia huduma hiyo muhimu.

Akizungumza juzi wakati wa hafla ya uzinduzi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Zawa, Mussa Ramadhan, alipongeza hatua hiyo akieleza kuwa, itasaida katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wateja visiwani Zanzibar.

“Mkakati wetu ni kuendeleza na kutoa huduma ya maji ya uhakika na nafuu kwa wateja wetu, hivyo ushirikiano wetu na Ezypesa utasaidia katika kufikia malengo yetu kwani utaongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato na kuwapunguzia wateja mzigo wa kutembea umbali mrefu kwani kwa sasa kila kitu kitafanyika kwa simu,” alisema.


Ramadhani alisema huduma hiyo ni suluhisho katika kuongeza kasi na ufanisi wa ukusanyaji wa mapato hivyo kusaidia mamlaka kuwa na uwezo wa kuboresha miundimbinu ya maji na kuwafikia watu wengi zaidi.


 Kwa upande wake, Mkuu wa Zantel-Zanzibar, Khamis Mussa, alisema hatua hiyo ni muhimu katika kutekeleza mkakati wa Zantel wa kuboresha maisha ya watu kupitia huduma za Ezypesa, ambazo zinawapa wateja wake uhuru na urahisi wa kupata huduma mbalimbali.


“Kupitia Ezypesa tumejizatiti katika kuboresha maisha ya watu kwenye nyanja mbalimbali, ili kuwezesha urahisi wa upatikanaji wa huduma na mahitaji ya kila siku. Ushirikiano wetu na ZAWA ni hatua muhimu katika kuhakikisha wateja wetu wanalipia ankara za maji mahali popote,” alisema Mussa.


 “Tofauti na njia za awali, kwa sasa hakuna haja tena ya kutembea umbali mrefu, ili kulipia bili au kusubiri mpaka maji yakatike kwa kuchelewesha bili, kwa simu yako tu unaweza kujihakikisha unapata huduma ya maji,” aliongeza.


Alisema ni dhahiri kuwa maji ni rasilimali muhimu katika kuchochea huduma za kibiashara pamoja na zile za majumbani na mamlaka ya maji Zanzibar (ZAWA) inafanya jitihada kubwa kusimamia huduma ambayo hadi sasa imewafikia wateja 1,161,915 visiwani Zanzibar.