Biteko kufungua soko la kimataifa la madini

15Jun 2019
Na Mwandishi Wetu
ARUSHA
Nipashe
Biteko kufungua soko la kimataifa la madini

WAZIRI wa Madini, Dotto Biteko, leo anatarajia kufungua soko la kimataifa la madini katika jijini Arusha, likiwa ni la pili baada ya la mpakani mwa Tanzania na Kenya katika eneo la Namanga.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, aliiambia Nipashe mjini hapa kwamba soko hilo litakuwa katika jengo ambalo hapo awali lilikuwa likitumiwa na shule ya Braeburn katika barabara ya Old Moshi.

 

 

 

"Hatua ya kufungua soko hilo imezingatia mahitaji ya wadau wa madini kwa maana wachimbaji wa madini, wanunuzi wakubwa na wafanyabiashara wa kimataifa kutoka nchi mbalimbali ambako shughuli kufanyikia hapo ni rahisi kwao, usalama wa uhakika na miundombinu muhimu yote ipo," alisema.

 

Gambo alisema kuwa soko hilo litakuwa umbali mfupi kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), eneo lenye huduma zote za kibenki na hoteli ya ngazi mbalimbali.

 

Kaimu Ofisa wa Madini Mkazi wa Arusha, Robert Erick, alisema uamuzi wa kufungua soko la kimataifa la madini jijini Arusha unatokana na mji huo kuwa kitovu cha madini ya aina mbalimbali ya vito.

 

Erick alisema soko hilo ni la pili kuanzishwa mkoani Arusha baada ya mwezi Aprili, mwaka huu, kufunguliwa soko lingine katika eneo la Namanga ambako ni mpakani mwa Tanzania na Kenya.

 

Alisema soko hilo la Namanga limekuwa likifanya kazi katika siku zote za kazi kuanzia Jumatatu mpaka Ijumaa na imewalazimu wadau wa madini kusafiri kutoka mjini kwenda umbali wa zaidi ya kilometa 100.

 

Akifafanua faida ya kuwapo kwa masoko hayo, Erick alieleza kuwa kwa kiasi kikubwa imepunguza utoroshaji wa madini kupitia njia za panya pamoja na urasimu kwa wauzaji na wanunuzi wa madini.

 

Aidha, Erick alisema kuwa utaratibu huo umerahisisha upatikanaji wa kodi za serikali pamoja na ukusanyaji wa takwimu za madini.

 

"Ni mfumo ambao unawasaidia hata wanunuzi na wauzaji kutapeliwa kama ilivyo kuwa siku za nyuma, lakini pia kuwaondolewa usumbufu wa kuzunguka kutoka ofisi moja hadi nyingine na pia kutusaidia kukusanya maduhuli ya serikali," aliongeza.

 

Baadhi ya madini ya vito yanayopatikana mkoani Arusha ni pamoja na Tanzanite, Sapphire, Emarald, Tourmaline, Aguamarine, Zircon, Garnet, Arnethyst, Rhodolite na Alexandrite.

 

Ufunguzi wa masoko ya madini katika maeneo mbalimbali unatokana na agizo la Rais John Magufuli, alilolitoa Aprili 27, mwaka huu alipokuwa wilayani Chunya.

 

Akiwa wilayani humo, Rais Magufuli alitoa siku saba kwa wakuu wa mikoa yote yenye shughuli za uchimbaji wa madini kuhakikisha wanafungua masoko hayo.

Habari Kubwa