Biteko awapa mtihani wachimbaji wadogo

06Jul 2019
Mohab Dominick
SHINYANGA
Nipashe
Biteko awapa mtihani wachimbaji wadogo

WAZIRI wa Madini, Doto Biteko, amekabidhi leseni kwa vikundi  23 vya wachimbaji wadogo wadogo wa dhahabu wa Mwakitolyo wilayani Shinyanga huku akiwataka kufuata sheria na masharti ya uchimbaji .

WAZIRI wa Madini, Doto Biteko.

 

Wananchi waliokabidhiwa leseni hizo ni wale waliokuwa wakichimba dhahabu katika eneo la Nyaligongo, Kata ya Mwakitolyo. Eneo hilo lilikuwa likimilikiwa na mgodi wa Acacia zamani Barrick.

Waziri Biteko alikabidhi leseni hizo juzi kwa wachimbaji hao alipofanya ziara ya kikazi kwa lengo la kutekeleza agizo la ugawaji wa leseni za uchimbaji lililotolewa na Rais John Magufuli.

Alisema kuwa kufuatia kupatikana kwa leseni hizo na kuelekezwa kupitia mafunzo waliyopatiwa wachimbaji wote wahakikishe kila baada ya mwezi mmoja wanawasilisha taarifa ya uzalishaji kwa mujibu wa kifungu cha 101 cha Sheria ya Madini ya 2010 na marekebisho yake ya 2017 na kifungu cha 16(1) cha kanuni za Madini cha mwaka 2018.

 

Aliwaagiza wachimbaji hao kuhakikisha wanafuata masharti ya leseni zao ikiwa ni pamoja na kulipa malipo ya Mrabaha unaotokana na uzalishaji wa Madini katika leseni zao kwa mujibu wa kifungu cha 87 cha sheria ya Madini 2010  na marekebisho yake 2017, pamoja na kifungu cha 90 (a)3 cha sheria ya fedha cha mwaka 2001 na marekebisho yake mwaka 2017.

Aidha, Waziri Biteko alisema kazi ya serikali kupitia Wizara ya Madini ni kuwalea wachimbaji wadogo ili kukua na kuondokana na uchimbaji mdogo na kuongeza kuwa haiwezekani watu kutoka Congo na Msumbiji walete madini yao kwenye masoko ya Tanzania.

"Mchukieni mtu anayetorosha madini. Mkimuona toeni taarifa, nafurahi pale  Watanzania wengi wanatoa taarifa za mtu anayetorosha madini, vile vile kila mtu awe mlinzi wa mwenzake. Ninyi mpo mnaosha kwa kutumia mekyuri hata tajiri nae muulizeni umeuza lini? umeuza wapi?. Akikufukuza kwa kuhoji nitumie ujumbe  nitashughulika naye,” alisema.

Pia Waziri huyo aliwaeleza kuwa mgodi huo kabla ya kupewa leseni hizo, haukuwa na tija yoyote ile na ni miaka mitatu sasa na rekodi zinaonyesha kuwa kiwango cha kodi ni sifuri hali ambayo aliwapa mtihani wa kukusanya kodi baada ya kumilikishwa kihalali.

Naye Mbunge wa Jimbo la Solwa, Ahmed Salum, alimweleza waziri kuwa wachimbaji walitii kauli ya Rais Magufuli ya kuwataka wasiondoke katika maeneo yao ya uchimbaji kutokana na agizo la ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kuwataka waondoke ili kumpisha mwekezaji mkubwa, kampuni ya Acacia anayedaiwa ndiye mmiliki wa eneo hilo.

Mwekezaji huyo anadaiwa alilishikilia kwa muda mrefu eneo hilo bila kuliendeleza hali iliyosababisha serikali kutoa leseni kwa wachimbaji wadogo kuendelea na uchimbaji.

Mbunge huyo aliwataka wachimbaji hao kutumia fursa hiyo ya leseni za uchimbaji  kufanya kazi kwa kujituma na kumuunga mkono Rais Magufuli kwa kulipa mirabaha ya serikali  huku  akiwasihi kutouza maeneo yao kwa kuwa serikali imeanza kuweka miundombinu muhimu kama elimu, barabara, umeme na maji.

Habari Kubwa