Bodaboda wakiri kutumiwa na wanasiasa

09Sep 2016
Jaliwason Jasson
BABATI
Nipashe
Bodaboda wakiri kutumiwa na wanasiasa

MADEREVA bodaboda wilayani Babati wamekiri kutumiwa na wanasiasa kuipinga serikali na sasa wameahidi kubadilika na kutoa ushirikiano kwa serikali.

madereva bodaboda wa mjini Iringa.

Waendesha bodaboda hao walitoa kauli hiyo kjana baada ya Mkuu wa Wilaya ya Babati, Raymond Mushi, kuzindua ofisi ya Umoja wa Waendesha Pikipiki Babati (Uwapiba) na kufunga mafunzo ya madereva hao wapatao 200.

“Tulikuwa tunatumiwa sana na wanasiasa, sasa tumebadilika hatukubali tena kutumiwa katika kufanya vitendo vya kuipinga serikali na kutofuata sheria.’’

"Hatuwezi kuendelea kutumiwa kama mtaji wa wanasiasa ambao baada ya kumaliza uchaguzi wanaangalia maisha yao na familia zao na kututelekeza," alisema mwenyekiti wa madereva hao wa bodaboda mkoa wa Manyara, Mussa Issa.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Mushi alisema kuanzishwa kwa ofisi hiyo ni kuirahisishia serikali kazi kwa kua itakuarahisi kuwasaidia tofauti na kipindi cha nyuma.

“Sisi kama serikali tutawasaidia ofisi yenu iwe ya kisasa na iwe na mfumo wa kielektroniki, tutatengeneza mfumo utakaowaunganisha na polisi ili ikitokea mtu amepata ajali au ualifu tuweze kujua kirahisi pamoja na kuona picha yake.’’

"Kinachotakiwa ni maendeleo lakini hoja kubwa ni nidhamu katika kufanya kazi na kuzitii sheria za nchi," alisema.

Naye Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Manyara, Mary Kipesha, aliwataka waendesha bodaboda kuzingatia sheria za usalama barabarani na kuwashauri wasiishie kufanya kazi hiyo tu bali waanzishe miradi mingine ya kujiongezea kipato.

“Wewe ukifuata sheria hutafuatwafuatwa, usipoifuata utakuwa mtumwa wa hiyo sheria, maana utaadhibiwa na kulazimishwa kuzifuata,’’ alisema.

Kwa upande wake, mkurugenzi wa taasisi isiyo ya kiserikali ya Apec, Respicios Timanywa, alisema waendesha bodaboda waliopata elimu hiyo wakikiuka sheria za usalama barabarani wasitozwe faini na polisi, badala yake wafikishwe mahakamani moja kwa moja.

Habari Kubwa