Bodaboda wapewa neno kujikwamua kiuchumi

20Jan 2019
Neema Sawaka
 KAHAMA
Nipashe Jumapili
Bodaboda wapewa neno kujikwamua kiuchumi

BARAZA la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC),  limewashauri waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda, kuanzisha vikundi ili kupata mikopo katika taasisi mbalimbali za fedha na hatimaye kuanzisha miradi mingine ya kujiongezea kipato.

Bodaboda

Asilimia kubwa ya waendesha bodaboda hapa nchini, wanaendesha pikipiki za matajiri na wanashindwa kujikwamua kiuchumi kutokana na mapato wanayoyapata kupelekwa kwa wamiliki.

Iwapo wataanzisha vikundi hivyo, imeelezwa kuwa wanaweza kukopeshwa fedha ambazo zitawasaidia kufungua miradi ya maendeleo pasipo kutegemea pikipiki.

Mratibu wa Mifuko na Programu za Uwezeshaji wa NEEC, Nyakaho Mahimba, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini hapa.

Alisema kuwa madereva wengi wa bodaboda hawaweki akiba lakini wakiwa katika vikundi wanaweza kukopesheka na kufungua miradi mingine tofauti na bodaboda utakaokuwa ukiwaingizia kipato hivyo kubadilisha maisha yao.

Pia alisema lengo la NEEC ni kuwawezesha madereva wa bodaboda kufanya shughuli hiyo kwa lengo la kutafuta mtaji huku fedha hizo zikipatikana, wahamie kwenye shughuli zingine za uzalishaji mali, jambo ambalo hawatakuwa tegemezi pale umri unapoenda na wakati watakapokuwa hawawezi kuendelea na kazi ya udereva wa bodaboda.

“Sisi baraza la taifa la uwezeshaji wananchi kiuchumi lengo letu ni wananchi na wajasiriamali wajikwamue kiuchumi kwa kutumia fursa zinazotolewa na serikali hususan mikopo inayotolewa na serikali yenye masharti nafuu,” alisema Mahimba.

Akizungumza kwa niaba ya madereva pikipiki wilayani Kahama, Mwenyekiti wa Kituo cha Pikipiki cha JVC, Husein Kakoba, alisema suala la kujiunga katika vikundi ni zuri kwa kuwa asilimia 80 ya madereva wa bodaboda, pikipiki wanazoendesha si zao, hivyo wakipatiwa fursa ya kupata mikopo ya masharti nafuu watainuka kiuchumi.

Aidha, alisema bodaboda wengi hawana nyumba au maeneo wanayoyamiliki ili kuwawezesha kupata mikopo katika taasisi za fedha, hivyo kuwa na kikundi chenye usajiri wa kuaminika pamoja na elimu, vitawasaidia kujitambua na itakuwa njia ya  kupiga hatua kimaendeleo.

Habari Kubwa