Bodi ya Barabara yakusanya bil. 360/-

14Jan 2018
Renatha Msungu
Nipashe Jumapili
Bodi ya Barabara yakusanya bil. 360/-

BODI ya Mfuko wa Barabara Nchini, imekusanya Sh. billion 360.2 kwa  mwaka  2017/2018 kutokana na tozo ya kodi ya magari na mafuta. 

Hayo yalisemwa na  Kaimu Meneja wa Bodi hiyo, Rashid Kalimbago, wakati akitoa ripoti kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandika, mkoani hapa. 

Kalimbago alisema makusanyo hayo yanatawanywa katika sehemu mbalimbali kwa ajili ya matumizi ya barabara ikiwamo ujenzi. 

Alisema lengo ni kukusanya zaidi ya hapo kwa sababu wanahitaji kufanya marekebisho ya barabara nyingi hapa nchini. 

Alisema tozo ya mafuta ni chanzo kikuu cha mapato ya mfuko, ambapo huchangia asilimia 97 ya mapato yote ya mfuko huo. 

Alifafanua zaidi kuwa tozo ya magari ya kigeni ni asilimia moja ambapo tozo hiyo hukusanywa na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA). 

Alisema ufanisi wa vyanzo hivyo unategemea mambo mengi ikiwa ni pamoja na usalama nchini na ubora wa barabara zilizopo. 

Alisema tangu bodi hiyo ianzishwe wamepata mafanikio makubwa sana kutokana na kufanya kazi kwa weredi mkubwa. 

Aidha, aliwataka wananchi kutoa taarifa pale wanapokuta barabara zinaharibiwa ili wachukue hatua stahiki kwa wahusika. 

Alisema mtandao wa barabara umeimarika kwa kiasi kikubwa tangu wakala wa barabara zianze kupata fedha za mfuko huo. 

Aliongeza kuwa barabara za wilaya zilizo katika hali nzuri zimeongezeka kwa asilimia 57 mwaka 2016/2017. 

Habari Kubwa