Bodi ya Kahawa kutafuta wanunuzi binafsi

04Jun 2020
Na Mwandishi Wetu
Mara
Nipashe
Bodi ya Kahawa kutafuta wanunuzi binafsi

BODI ya Kahawa imetakiwa kutafuta wanunuzi binafsi kadri iwezavyo ili kuongeza ushindani lengo ni wakulima wauze kahawa kwa bei nzuri isiyokandamizi.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, alipokuwa akizungumza kwenye kikao kazi na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa, Prof. Jamali Adam.

Alisema wanunuzi  binafsi wataruhusiwa kununua kahawa kupitia vyama vya ushirika badala ya kwenda moja kwa moja kwa wakulima.

Alibainisha hatua hiyo itasaidia kukabiliana na unyonyaji dhidi ya wakulima wa kahawa pamoja na mazao mengine mkoani Mara.

"Mkulima yeyote akisikia bei nzuri ya kahawa lazima atauza…hawezi kwenda kwenye bei ndogo wakati ameona kuna mahala kuna bei nzuri inayoendana na jasho lake,” alisema.

Alisema serikali iliamua kuanzisha ushirika kwa ajili ya wakulima kuuza mazao yao kwa bei nzuri, hivyo wanunuzi binafsi ni ruksa, lakini wanapaswa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.

"Uuzaji wa Mazao ya wakulima kupitia vyama vya ushirika tumeuweka ili kama wakulima wakiibiwa au kupunjwa…sisi iwe rahisi kumpata muhusika na tunachukua hatua kali dhidi ya wote watakaofanya ubadhirifu, lakini tukimkuta mnunuzi binafsi ameingia mpaka shambani ni kama ameingia chumbani atapata balaa," alisisitiza Malima.

Sambamba na hilo, aliipongeza bodi hiyo kwa kutoa miche 40,000 kwa ajili ya mkoa wa Mara, huku akisisitiza umuhimu wa bodi hiyo kuwaongezea wakulima miche mingi zaidi ili kuongeza uzalishaji wa kahawa nchini.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi, Prof. Adam, alisema kuwa bodi imejiwekea malengo muhimu ya kuongeza uzalishaji wa kahawa nchini, na kuwa na bei nzuri.

Habari Kubwa