Bodi ya Vileo yatakiwa kung’oka

26Jan 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Bodi ya Vileo yatakiwa kung’oka

VIONGOZI wa Bodi ya Udhibiti na Ushauri wa Vileo Zanzibar wametakiwa kujiuzulu baada ya kutoa vibali kwa kampuni sita kuingiza pombe badala ya tatu kwa mujibu wa sheria mpya namba 9 ya mwaka 2020.

Wito huo ulitolewa na wanaharakati wa haki za binadamu na wanasheria walipokuwa wakizungumzia mgogoro wa sheria namba 9 ya mwaka 2020 baada ya kuanza kutumika Januari mwaka huu na kusababisha mfumuko wa bei ya vileo Zanzibar.

Wakili maarufu Zanzibar,  Rajab Abdallah, alisema kwa mujibu wa kifungu cha 33 (1) kimeeleza kibali cha kuingiza vileo kitatolewa kwa waangizaji wasiozidi watatu kwa kuzingatia masharti kwanza mhusika awe Mzanzibari, awe mlipakodi, awe na ghala la kuhifadhia pamoja na gari maalum la kusambaza vinywaji vyake.

“Kitendo cha kuweka kando sheria na kutoa vibali kwa kampuni sita badala ya tatu ni uvunjaji wa sheria na Mwenyekiti wa Bodi anapaswa kujiuzulu kwa kuvunja sheria,” alisema Wakili Rajabu.

Alisema Zanzibar inaongozwa kwa misingi ya utawala wa sheria na hakuwa mwafaka kwa Mwenyekiti wa Bodi kutumia hekima na busara kuongeza idadi ya kampuni kwa madhumuni ya kulinda maslahi mapana ya serikali ya kukusanya kodi.

Rajab alisema kabla ya sheria kupitishwa na Baraza la Wawakilishi na kuanza kutumika baada ya kusainiwa na Rais wa Zanzibar Mei mwaka 2020 mapendekezo ya sheria yalijadiliwa na wadau wa vileo, makatibu wakuu pamoja na Baraza la Mawaziri kabla ya muswada wa sheria kupelekwa barazani.

“Mwenyekiti wa Bodi anataka kutuambia viongozi wote waliojadili sheria hii wakiwamo makatibu wakuu, wawakilishi na Baraza la Mawaziri wakiongozwa na rais hawakuona maslahi mapana ya mapato ya serikali mpaka wakaweka ugomo wa idadi ya kampuni za kuingiza pombe mwisho tatu kwa mujibu wa sheria,” alihoji Wakili Rajabu.

Alisema kampuni zote zilizopewa vibali vya ziada zitakuwa zinafanya biashara kinyume cha sheria kwa vile vibali walivyopewa sawa na karatasi kwa sababu vimetolewa kinyume cha sheria.

Kwa upande wake Mwanaharakati wa Haki za Binadamu na Utawala Bora, Ali Makame Issa, alisema maamuzi yaliyofanywa na Bodi ya Vileo yanakwenda kinyume cha misingi ya utawala bora.

“Nchi inaongozwa kwa kufuata katiba na sheria, sio hekima na busara ndio maana kunatungwa sheria na hakuna mamlaka yoyote yenye ubavu wa kuvunja sheria,” alisema Issa.

Alisema kama kutafuta mapato serikali ingelikuwa na uwezo wa kuuza dawa za kulevya au kutakatisha fedha, lakini haiwezi kufanya hivyo kwa sababu ni kinyume cha sheria.

Hata hivyo, alipoulizwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Mwinyi Talib Haji, kuhusu mvutano wa vibali vya kampuni za uingizaji wa vileo hakutaka kuzungumza chochote.

Mwenyekiti wa Bodi ya Udhibiti na Ushauri ya Vileo Zanzibar, Abdulrazaki Abdulkadiri, alisema mtu yeyote ambaye anaona sheria imevunjwa yuko huru kwenda mahakamani.

“Bodi kweli tumeongeza kampuni zaidi ya tatu kwa baada ya kuzingatia maslahi mapana ya serikali katika ukusanyaji wa mapato na kampuni ambazo zilikuwa zimekosa ni walipaji wakubwa wa kodi kupitia vileo,” alisema.

Naye Kiongozi Mwandamizi wa Taasisi ya Kiislamu Zanzibar, Sheikh Abdalla Hussen, alisema malengo ya kutungwa sheria mpya ya vileo imelenga kudhibiti biashara ya pombe kufanyika kiholela katika mitaa pamoja na maeneo ya huduma za jamii.

Alisema bodi inapaswa kuchunguzwa kutokana na maamuzi waliyofanya kutokana na kuvunja sheria kinyume cha madhumuni ya kutungwa sheria ya kudhibiti na kusimamia vileo.

Habari Kubwa