Bodi yafurahishwa ujio ATM maziwa

22Oct 2019
Na Mwandishi Wetu
Moshi
Nipashe
Bodi yafurahishwa ujio ATM maziwa

KAIMU Msajili wa Bodi za Maziwa Nchini, Sofia Mlote, ameeleza kufurahishwa na ujio wa teknolojia mpya ya ununuzi wa maziwa kwa njia ya mashine za ATM.

Mlote alisema ujio wa mashine hizo utarahisisha wananchi wa Kilimanjaro kunywa kiwango sahihi cha maziwa ambacho ni lita 200 kwa mwaka kwa mtu.

Alieleza imani yake hiyo jana, wakati wa mahojiano na Nipashe kuhusu teknolojia mpya mashine za ATM za maziwa ambazo zimewekwa katika wilaya za Hai na Manispaa ya Moshi.

Alisema kwa sasa Mtanzania anakunywa lita 49 za maziwa kwa mwaka, wakati anatakiwa kunywa lita 200.

Alisema kazi ya bodi ni kusimamia sheria na kanuni za uzalishaji wa maziwa pamoja na wadau wanaozalisha chakula hicho nchini na kwamba uzalishaji ni lita bilioni 2.7 kutoka ng'ombe wa maziwa milioni 1.294.

Alisema kutokana na uzalishaji huo, asilimia 10 ndizo zinazokwenda kwenye mfumo rasmi za usindikaji wa maziwa na kwamba asilimia 90 inaenda kwenye mifumo isiyo rasmi.

Alisema usindikaji ni lita 154,000, lakini mikakati ni kusindika zaidi ya lita 815,000 za maziwa, na kwamba bado uhitaji upo kwa kuwa maziwa yanayoingizwa nchini kwa mwaka ni lita milioni 20.

"Kunatakiwa nguvu ya pamoja ya kuundwa kwa vikundi vya ushirika ili kuweza kutetea na kusimamia kinachoaminiwa na wadau wa tasnia ya maziwa ili kuweza kufikia mbali," alisema.

Aidha, alisema kila mwanachama wa ushirika lazima awe na shamba la malisho, ili kuwapa mifugo chakula bora pamoja na kupata maziwa salama yakutosha.

Kutokana na mafanikio hayo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dk. Anna Mghwira, aliwataka maofisa ugani kuwafikia wazalishaji walipo ili waweza kupata mbegu bora za ng’ombe zinzaozalisha maziwa yaliyo bora.

Alisema sambamba na upatikanaji wa maziwa, pia wafugaji wahamasishwe kunywa maziwa na si kuuza yote kama walivyozoea.

Mkurugenzi wa Match Maker, Peniel Uliwa, alisema, mradi huo wa Faida Maziwa umefadhilia na Shirika la Maendeleo ya Uholazi (SNV) kupitia Match Maker Associate, ambao umewapatia vikundi mashine za kuchakata chakula cha mifugo pamoja na teknolojia mpya na ya kwanza hapa nchini ya milk ATM.

Alisema mitambo hiyo inabeba lita 300 na kwamba ATM inagharimu Sh. milioni 19 na zimepatiwa kwa mikundi viwili vya vijana ambao ndiyo watakaosimamia mradi huo.