Bonite Bottlers kutoa msaada wa madawati Karatu

07Mar 2017
Asraji Mvungi
ARUSHA
Nipashe
Bonite Bottlers kutoa msaada wa madawati Karatu

KAMPUNI ya kutengeneza vinywaji baridi vya jamii ya Coca Cola ya Bonite Bottlers Ltd, imeanza mchakato wa kutoa msaada wa madawati kuzisaidia baadhi ya shule za Wilaya ya Karatu, mkoani Arusha zinazokabiliwa na tatizo hilo.

Akizungumza katika hafla ya kupokea awamu ya kwanza ya msaada huo wa madawati hayo kutoka kampuni hiyo,

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Karatu, Waziri Mouris, aliishukuru kampuni hiyo kwa kuguswa na tatizo hilo na aliwaomba wadau wengine pia kuona umuhimu wa kusaidia sekta ya elimu.

"Tunawashukuru sana Kampuni ya Bonite, madawati haya yamekuwa ni msaada mkubwa sana kwetu, yamepunguza pengo kubwa tulilonalo la madawati, tunawaomba na wengine waone umuhimu wa kusaidia,” alisema.

Ofisa Elimu wa Wilaya ya Karatu, Papakinyi Kaai na baadhi ya walimu akiwamo Zaina Thabiti, walisema msaada huo umeongeza hamasa kwao wenyewe na pia kwa wanafunzi na ni ukombozi mkubwa kwa watoto waliokuwa wanashindwa kuzingatia masomo kwa sababu ya kusongamana.

Mratibu wa mauzo wa kampuni hiyo, Kanda ya Manyara na Karatu, Joseph Simplisi, alisema kampuni hiyo itaendelea kujitolea kuchangia na kuisaidia jamii katika kutatua changamoto za elimu ikiwa ni sehemu ya kurejesha kwa wananchi faida inayotokana na bidhaa zake.

“Huku kwenye jamii ndiko wanakopatikana wateja wa bidhaa zetu na pia huku ndiko wanapatikana viongozi wa kesho, wafanyakazi na watendaji wa kesho hivyo wataendelea kusaidia kadiri watakavyoweza,” alisema.

Habari Kubwa