Bosi wa TCRA ahimiza vijana uchumi kidigitali

16Oct 2020
Grace Mwakalinga
Mbeya
Nipashe
Bosi wa TCRA ahimiza vijana uchumi kidigitali

MKUU wa Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Asajile John, amewataka vijana kutumia vyema teknolojia za mawasiliano hususani TEHAMA katika shughuli za uzalishaji, ili kulisaidia taifa kufikia uchumi wa kidigitali.

Asajile alitoa rai hiyo juzi wakati wa kongamano lilowahusisha vijana wa shule za sekondari na vyuo kutoka maeneo mbalimbali ya Jiji la Mbeya kwenye Siku ya Kumbukizi ya Kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, lililoandaliwa na Shirika la Lightness Tanzania.

Alisema vijana wanapaswa kuenzi falsafa ya Hayati Mwalimu Nyerere ya kujitegemea kwa kuhakikisha wanatumia teknolojia za mawasiliano kujiletea maendeleo ikiwa ni pamoja na kutumia kwenye shughuli za biashara, kilimo na wanafunzi kujisomea na kutafuta ajira.

“Kifo cha Mwalimu Nyerere kinatukumbusha Watanzania kuyaenzi na kuyafanya yale aliyoyaagiza kama vile falsafa ya uhuru wa kujitegemea kwa kuhimiza watu waendelee kufanya kazi kwa bidii na alijitahidi kuboresha miundombinu ya mawasiliano katika kila pembe ya nchi,” alisema.

Asajile alisema lengo la TCRA ni kuhamasisha vijana kutumia kwa manufaa yao kama vile kufahamu mabadiliko mbalimbali yanatokea duniani na kuwa makini na matumizi ya TEHAMA ili kujiepusha na uvunjifu wa sheria za mitandao.

Akifungua kongamano hilo, Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Tanzania (TIA) Tawi la Mbeya, Dietrich Mgaya, alipongeza awamu mbalimbali za uongozi wa nchi kwa kuendelea kuziishi falsafa za Hayati Mwalimu Nyerere kwa kutoa huduma bora za jamii katika masuala ya afya, elimu, umeme na maji.

Sambamba na hayo, Mgaya pia aliwapongeza viongozi hao kwa kudhibiti matumizi mabaya ya rasilimali za umma pamoja na kujenga miundombinu wezeshi kwa ajili ya uwekezaji.

Mkurugenzi wa Shirika la Lightness Tanzania Organization, Aliko Brown, alisema wanajihusisha na shughuli za kuongeza maarifa kwa jamii na kuwahamasisha waendelee kujitegemea kwa kubuni na kuanzisha shughuli mbalimbali za kuwaingizia kipato.

Alisema falsafa ya uhuru wa kujitegemea kama ajenda yao katika kumuenzi Mwalimu Nyerere, inawakumbusha vijana kujiamini, kuwa wabunifu na kufanya utafiti ili ulete tija kwa taifa.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari St. Marry’s, Cornelius Mtambo, alisema moja ya jukumu walilonalo ni kuwaandaa wanafunzi kujitegemea kabla na baada ya kumaliza masomo yao.

Habari Kubwa