CEED Tanzania yawapa mbinu wajasiriamali kukuza biashara zao

09Oct 2019
Mary Geofrey
Nipashe
CEED Tanzania yawapa mbinu wajasiriamali kukuza biashara zao

KITUO cha Ujasiriamali na Maendeleo ya Utendaji (CEED), kimewakutanisha wajasiriamali mbalimbali jijini Dodoma katika semina iliyolenga kutoa elimu ya usimamizi na ukuzaji biashara zao ndani ya jiji hilo.

elizabeth Swai akizungumza uzoefu wake wakati wa semina ya CEED Tanzania Dodoma

Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki, mwakilishi kutoka CEED Tanzania Fred Laiser, amesema semina hiyo ni kwa ajili ya kuwapa ujuzi  wa namna ya kuboresha biashara zao, ushindani wa kusaka fursa mbalimbali kutoka na kuongeza kwa idadi kubwa ya watu baada ya Serikali kuhamishia shughuli zake Dodoma.

“Sisi CEED Tanzania lengo letu kuu ni kuwasaidia wajasiriamali nchini kukuza biashara zao. Leo tupo hapa Dodoma kwa lengo kuwapa elimu na kutoa fursa mbalimbali za kibiashara ambazo wajariamali wanaweza kuzichangamkia. Pia kuwakutanisha na wenzao wajifunze namna ya kukuza biashara zao, kutatua changamoto zao,’’Laiser alisema.

Mbali na hilo, Fred Laiser alitumia nafasi hii kuwataka wajasirimali mbalimbali nchini kujitokeza kwa wingi katika semina mbalimbali za ujasiriamali hasa zinazoendeshwa na CEED Tanzania kwaji ajili ya kupata ujuzi wa biashara zao na pia kufahamiana na wajasiriamali kutoka kila kona ya Tanzania.

Kwa upande wa wanufaikaji wa mafunzo hayo, Mwanzilishi wa Kampuni ya Ufugaji kuku ya AKM Glitters Limited, Elizabeth Swai,  alisema wana fursa na fursa mbalimbali ingawa pia wana changamoto katika ukuzaji wa biashara zao.

 “Nawapongeza sana CEED Tanzania kwa kutupa nafasi hii ya kujifunza na kukutana na wajasiriamali wenzetu ili kujifunza mambo mbalimbali kutoka kwao.

Moja ya changamoto inayotukabili sisi wajasiriamali hapa nchini ni kushindwa kuendeleza biashara zetu mara baada ya kuanzisha. Wengi tunapenda kujiajiri lakini wachache ndio wanaofikia malengo yao.Ili kutatua changamoto hizi inatupasa kujifunza vitu vipya kila siku na kujaribu mara kwa mara mpaka pale biashara itakapoweza kujiendesha yenyewe,” Swali alisema.

Habari Kubwa