Chanzo migogoro ya wanyama, watu chawekwa bayana

15Jan 2022
Renatha Msungu
Dodoma
Nipashe
Chanzo migogoro ya wanyama, watu chawekwa bayana

ONGEZEKO la idadi ya watu nchini na mahitaji ya ukuaji imechangia kwa kiasi kikubwa migogoro kati ya binadamu na wanyamapori kutokana na kugombea maliasili zilizopo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Dk. Cecilia Leweli kutoka Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) migogogoro kati ya binadamu na wanyamapori imesababisha hasara kubwa za kijamii, kiuchumi na kibioanuwai pamoja na uhifadhi wa wanyamapori.

Alisema kuingiliwa kwa makazi ya wanyamapori pamoja na shoroba kunatishia uhusiano wa kiikolojia wa maeneo yaliyohifadhiwa.

“Migogoro kati ya binadamu na wanyamapori inatishia sana usalama wa makazi ya wanyamapori,” alisema Dk Leweri.
Alisema ushahidi wa kiutafiti unaonyesha kwamba kuna shoroba za wanyamapori ambazo katika ardhi za vijiji zinatumika kwa shughuli mbalimbali zikiwamo za makazi, kilimo na ufugaji.

“Ni dhahiri kuwa kukithiri kwa migogoro hii kunachangiwa kwa kiasi kikubwa na hali ya umaskini, ukosefu wa teknolojia na utekelezaji duni wa malengo ya kisekta.

Dk. Leweri alisema mapitio ya utafiti mbalimbali yanapendekeza kwamba ili kukabiliana na migogoro hiyo, kwanza ni lazima sera zote zinazohusiana na matumizi ya ardhi ziunganishwe kuhusu masuala yote ya matumizi ya ardhi.

Alisema mabadiliko chanya katika mtazamo wa jamii kuhusu uhifadhi wa wanyamapori katika maeneo mengi na kuimarishwa kwa shuhuli za uhifadhi nchini vimesababisha wanyamapori wengi kuwa huru na kuingia katika makazi ya watu, hivyo kusababisha uharibifu.

Mtaalamu huyo alisema kuwa ongezeko la wanyamapori si kubwa kiasi cha kusababisha madhara kwa watu na mali zao ikilinganishwa na miaka ya 1970 hadi 1990 ambapo idadi ya watu ilikuwa takribani million 30, huku idadi ya wanyamapori mfano tembo ikiwa 300,000.

Alisema wakati mwaka 2020 idadi ya watu ni milioni 60 idadi ya tembo ni takribani 60,000 na kubainisha kwamba ongezeko la tembo ni dogo ikilinganishwa na idadi ya watu.

Dk Leweri alisema ongezeko hilo limechangia kwa kiasi kikubwa kupanuka kwa miji na shughuli mbalimbali za kijamii kwa mfano kilimo na ufugaji zinazomwingizia mwanadamu kipato.

 

Habari Kubwa