China, SUA zawafunda maofisa ugani

12Jul 2018
Ashton Balaigwa
Morogoro
Nipashe
China, SUA zawafunda maofisa ugani

CHUO Kikuu cha Kilimo cha China kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia Wizara ya kilimo, kimeanza kutoa mafunzo maalumu kwa maofisa ugani wa kata na maofisa kilimo katika wilaya za mkoa wa Morogoro juu ya matumizi ya teknolojia rahisi katika uzalishaji.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Stephen Kebwe.

Mpango huo wa kuwafundisha maofisa ugani hao unakusudia kutoa elimu hiyo kwa ajili ya kuwaelimisha wakulima kuanzia ngazi ya chini, ili kutumia teknolojia hizo za kichina katika kilimo chenye tija na cha kibiashara.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, yanayowahusisha maofisa ugani, watafiti wa vyuo vya utafiti wa kilimo, wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha China, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Stephen Kebwe, alisema lengo ni kuongeza uzalishaji wa kilimo cha mahindi kutoka magunia manane kwa sasa hadi kufikia tani 4.5 kwa ekari moja.

Dk. Kebwe alisema mafunzo hayo yanafanyika baada ya kufanyika kwa mradi wa majaribio katika kijiji cha Peapea wilayani Kilosa na cha Mtego wa Simba katika wilaya ya Morogoro.

Katika mradi huo wa majaribio, wakulima walifundishwa kilimo cha mahindi kwa kutumia teknolojia rahisi na kufanikiwa kuongeza uzalishaji wake kutoka magunia manane hadi 15 kwa ekari.

Mkuu huyo wa mkoa alisema kutokana na matokeo hayo mazuri, vyuo hivyo viliingia makubaliano ya kuanzisha mradi wa kuwafundisha maofisa ugani, ili kueneza teknolojia hiyo kwa wakulima wa mkoa wa Morogoro ambao umekuwa ukichangia zaidi ya asilimia 50 kwenye ghala la taifa la chakula.

Naye Naibu Waziri wa Kilimo, Mary Mwanjelwa, alisema mafunzo hayo yatakuwa chachu ya kuwasaidia wakulima kulima kilimo chenye tija na cha kibiashara kwa kuwa tayari serikali imetangaza uchumi wa viwanda, huku asilimia 80 ya malighafi ikitarajiwa kutoka katika kilimo.

Mwanjelwa aliwaagiza maofisa ugani kote nchini kuacha kukaa ofisini na badala yake ofisi zao ziwe mashambani kutoa elimu kwa wakulima, ili kuongeza tija na uzalishaji wa mazao mbalimbali hasa katika kipindi hiki ambacho sekta ya kilimo ni tegemeo la malighafi katika uchumi wa viwanda.

Kwa upande wake, Mkuu wa Taasisi ya Uchumi na Biashara kutoka Serikali ya China, Lin Zhiyong, alisema kuwa wameguswa kusaidia Tanzania katika sekta ya kilimo kwa kuwafundisha wataalamu wa kilimo kujua matumizi ya teknolojia rahisi, ili kusonga mbele na kuingia katika uchumi wa kati ifakapo mwaka 2025.

Alisema ili kufanikisha mafunzo hayo, wameamua kuleta maprofesa tisa kutoka katika maeneo ya kilimo, sayansi ya chakula na uhandisi wa lishe na usimamizi wa uchumi.

Lin alisema China imepata maendeleo haraka kupitia sekta ya kilimo kutokana na matumizi hayo ya teknolojia na kwamba mpaka sasa kwa Tanzania zaidi ya wakulima 500 wameshapatiwa mafunzo hayo na kuongeza uzalishaji wa mahindi katika vijiji vya Peapea na Mtego wa Simba.

 

 

 

Habari Kubwa