Chunya kinara kuzalisha tumbaku bora

30Jun 2020
Nebart Msokwa
Chunya
Nipashe
Chunya kinara kuzalisha tumbaku bora

WILAYA ya Chunya mkoani Mbeya imetajwa kuwa ndiyo inayozalisha tumbaku bora kuliko maeneo yote nchini kutokana na wakulima wengi kufuata kanuni za kilimo bora cha zao hilo.

Hayo yalisemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Tumbaku Tanzania (TTB), Stanley Mnonzya, wakati wa uzinduzi wa masoko ya tumbaku nchini uliofanyika kitaifa katika Kata ya Lupatingatinga wilayani Chunya.

Alisema mikoa inayozalisha tumbaku nchini ni 12, lakini katika maeneo mengine wakulima hawafuati maelekezo ya wataalamu wa zao hilo hali ambayo inapunguza ubora, hivyo akawataka viongozi wa vyama vikuu vya ushirika kutoa elimu kwa wakulima wao.

“Mkoa wa kitumbaku wa Chunya unazalisha tumbaku bora sana, ni vyema mikoa mingine ikaja kujifunza huku ili tuzalishe tumbaku inayofanana kwa ubora katika maeneo yote,” alisema Mnonzya.

Alisema pamoja na ubora huo, lakini kuna tatizo la baadhi ya wakulima kushindwa kufuata sheria za kilimo cha zao hilo ikiwamo kuwatumikisha watoto kwenye mashamba na kutopanda miti ya kukaushia zao hilo.

Alisema hali hiyo inasababisha baadhi ya wanunuzi wa zao hilo kujitoa, na kwamba ili kudhibiti hali hiyo, TTB imeanza kuwaondoa kwenye daftari la usajili wakulima wanaobainika kukiuka taratibu hizo.

Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Maryprisca Mahundi, alisema pamoja na kwamba wilaya yake inasifika kwa uzalishaji wa tumbaku bora, lakini mwaka huu ubora huo umepungua kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Alisema mwaka huu kulikuwa na mvua nyingi kupita kiasi hali ambayo ilisababisha wakulima kushindwa kukausha zao hilo kwa ubora unaotakiwa.

“Tatizo lingine linalowakabili wakulima wetu ni bei kuwa chini kutokana na kuwa na mnunuzi mmoja ambaye hana ushindani wowote, tunaiomba wizara itusaidie kutafuta wanunuzi wengine,” alisema Mahundi.

Kwa upande wake Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, alisema baadhi ya wanunuzi wa zao hilo walikimbia soko la Tanzania na kukimbilia Zimbabwe, Malawi na mataifa mengine kutokana na matatizo mbalimbali yaliyojitokeza nchini kuanzia mwaka 2014.

Alisema kwa sasa baadhi ya matatizo hayo yametatuliwa na serikali na tayari wizara inaendelea na mazungumzo ya kibiashara na mataifa ya Misri na China ili yaje kununua tumbaku inayozalishwa  nchini.

"Wachina walisema wako tayari kuja kununua, lakini kwa masharti kuwa tuzalishe mbegu ya tumbaku wanayoitaka wao na walituletea tumeifanyia majaribio kule Kahama, lisingekuwa janga la corona wangekuwa wameshakuja sasa tunasubiri hali itulie," alisema Hasunga.

Aliwataka wakulima wa tumbaku nchini kuendelea kufuata taratibu za uzalishaji wa zao hilo ili kuepuka kukimbiwa na wanunuzi, huku akisisitiza kuwa serikali itaendelea kusimamia kilimo cha zao hilo la biashara.

Habari Kubwa