Chunya walilia mnunuzi tumbaku

09Oct 2019
Grace Mwakalinga
Chunya
Nipashe
Chunya walilia mnunuzi tumbaku

WAKULIMA wa tumbaku katika Halmashauri ya Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya wameiomba serikali kuwatafutia mnunuzi mbadala wa TLTC.

Kampuni ya TLTC iliyokuwa inanunua zao hilo imefungasha virago na kuondoka nchini ikiwaacha wakulima bila kujua hatima yao.

Wakizungumza na Nipashe juzi wakulima hao walieleza kuwa mpaka sasa tumbaku imejaa kwenye maghala na hakuna mnunuzi aliyejitokeza, hali inayoendelea kuwatia hofu kwamba huenda msimu ujao wa kilimo wakakosa fedha za kuhudumia mashambani.

Miongoni mwa wakulima hao Pius Lanzala alisema hadi sasa wamebaki njia panda kwani hawajui kama wataendelea na kilimo cha tumbaku au vinginevyo kwa sasa hawana mnunuzi mwingine mkubwa ambaye anaweza kununua mazao yao yakiwa ghalani.

“Tumbaku kwa ukanda wao ndiyo tegemeo katika kuendesha maisha ya familia zao na limewasaidia kujikwamua na umaskini hivyo kuondoka kwa mnunuzi wa kampuni ya TLTC kumeleta mashaka ya namna watakavyoishi,” alisema Lanzala.

Hata hivyo, Mbunge wa Lupa (CCM), Victor Mwambalaswa, alisema kuwa atafikisha kilio hicho kwa Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, ili kusaidia kutafuta mnunuzi mwingine mapema iwezekanavyo

Alisema kukosekana kwa mnunuzi mkuu wa zao hilo kumesababisha upenyo wa madalali na ‘makanjanja’ kuwalangua wakulima ambao hununua tumbaku hizo kwa bei ya chini.

Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Maryprisca Mahundi, alisema wanaendelea na jitihada za kutafuta masoko kupitia kampuni na wadau wa tumbaku, huku akitoa onyo kwa madalali kutotumia mwanya huo kuwalangua wakulima.

Alisema zao hilo ni miongoni mwa vyanzo muhimu vya mapato katika wilaya hiyo na kwamba wanafanya kila jitihada kuhakikisha wakulima wanapata mnunuzi wa uhakika.

Aliongeza kuwa endapo kilimo cha tumbaku kitasitishwa na wakulima kwa kukosa mnunuzi, Chunya itapata hasara ya zaidi ya Sh. bilioni moja ambazo ni fedha za makusanyo ya ndani zinazotokana na kodi ya zao hilo kwa mwaka.

Habari Kubwa