CMS yaongezea ujuzi uchimbaji wataalamu

08Sep 2021
Christina Mwakangale
Dar es Salaam
Nipashe
CMS yaongezea ujuzi uchimbaji wataalamu

KAMPUNI ya uchimbani madini ya CMS imewaongezea ujuzi wataalamu wake wa uchimbaji kwa kuwapa mafunzo ili kukidhi matumizi ya mfumo mpya katika kuchimba madini kielektroniki.

Mwenyekiti wa CMS Tanzania Limited, Balozi Ami Mpungwe, akizungumza hivi karibuni kuhusu uwekezaji wa mitambo mipya ya kielektroniki, alisema teknolojia hiyo ni ya kipekee kwenye uchimbaji wa chini ya ardhi barani Afrika.

Alisema kutokana na hilo timu maalum za uchimbaji na ufundi zimeandaliwa kwa ajili ya kutumia mifumo ya hali ya juu ya umeme ili kuongeza ufanisi zaidi kwenye utendaji kazi na hali ya usalama.

“Tunaimani na sekta ya madini nchini Tanzania kama iliyoweza kuonyeshwa kupitia jitihada endelevu za kujitoa kwetu kikamilifu kwa zaidi ya miaka 16. Kwa jinsi hii, tunaendelea kujizatiti katika kutoa teknolojia bora na yenye viwango kwa wateja wetu waliopo hapa.

“Uwekezaji mkubwa uliofanywa kwa ajili ya mtambo huu pamoja na mpango wa ujio wa mitambo mingine miwili nchini, mwaka huu, mtambo mmoja tayari upo njiani kuelekea kwenye mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu.”

Alisema tayari CMS imewekeza zaidi ya shilingi bilioni nane, kwenye mitambo ya Swick Gen II Mobile Drill kuunga mkono sekta ya madini nchini, imenunuliwa kwa ajili ya kuongeza ubora uchakataji wa madini, kuendeleza huduma za uchimbaji kwa kampuni ya Barrick kwenye mgodi wa Bulyanhulu.

“Mitambo hiyo mipya ni ya kwanza kuwahi kutumika barani Afrika, yenye uwezo mkubwa na teknolojia ya kipekee kwa ajili ya shughuli za madini pamoja na mifumo unayohakikisha usalama wa wafanyakazi wa uchimbaji katika kiwango cha hali ya juu.”

Pia, Mpungwe aliongeza kwamba kampuni imeanzisha vituo vipya mkoani Mwanza kwa ajili ya utekelezaji wa operesheni mbalimbali nchini vya kutengeneza na kuunda vifaa vingine huku ikiajiri Watanzania 418, wanaofanya kazi idara mbalimbali za biashara za kampuni hiyo.