CRB yataka makandarasi wakatae kutoa rushwa

26Sep 2021
Na Mwandishi Wetu
MWANZA
Nipashe Jumapili
CRB yataka makandarasi wakatae kutoa rushwa

MAKANDARASI nchini wametakiwa kutoa taarifa kwa Taasisi ya Kupambana na kuzuia Rushwa (TAKUKURU) wanapoombwa rushwa na watoaji wa zabuni ili wawawezeshe kupata miradi hiyo ya ujenzi.

Oscar Munisi ambaye ni mwenyekiti wa makandarasi Mkoa wa Mwanza akiteta jambo na Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Injinia Consolata Ngimbwa mara baada ya kufungwa kwa mafunzo ya siku tatu kwa makandarasi wazalendo kuhusu usimamizi wa fedha. Kushoto ni Naibu Msajili wa CRB, anayeshughulikia utafiti na maendeleo Injinia David Jere.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki mkoani Mwanza na Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi, Mhandisi Consolata Ngimbwa wakati akifunga mafunzo ya siku tatu kwa makandarasi wazalendo.

Alisema makandarasi hawapaswi kutoa rushwa wala kuwashawishi wengine kupokea rushwa kutoka kwao na kwamba iwapo watafanya kazi kwa weledi na maadili rushwa haitakuwa na nafasi kwenye shughuli zao za ujenzi.

“Tukikubali kubadilika wote tutaibadilisha na kuiboresha sekta ya ukandarasi hapa nchini hivyo nawasisitiza mjiepushe kabisa na vitendo vya kutoa na kupokea rushwa,” alisema

Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Injinia Consolata Ngimbwa akifunga mafunzo ya siku tatu kwa makandarasi wazalendo kuhusu usimaiizi wa fedha na masuala ya kodi yaliyofanyika ukumbi wa chuo cha Benki Kuu jijini Mwanza

Aliwataka makandarasi kushirikiana kupitia ubia kama njia ya kuwawezesha makandarasi wazalendo kupata fursa ya kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi.

Alisema kutimiza masharti ya miradi mikubwa ni vigumu kwa makandarasi wengi wanapokuwa mmoja mmoja lakini kwa mfumo wa ubia wanaweza kuyatimiza masharti hayo na kushinda zabuni.

Aliwataka makandarasi kuwa na chama kimoja kitakachokuwa sauti yao kwani sekta hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi ambazo haziwezi kutatuliwa kwa urahisi bila kuwa na umoja wenye nguvu.

Mtakumbuka kwamba nimekuwa nikilisema hili kwa muda mrefu sana mliohudhuria mikutano ya mashauriano ni mashahidi, umoja ni jambo ambalo nalisisitiza sana kote nchini na nafurahi nimekaa na wenyeviti wa vyama vya makandarasi nao wameona umuhimu huo, “ alisema Injinia Ngimbwa

Naye Naibu Msajili wa (CRB) anayeshughulikia Utafiti na Maendeleo, Injinia David Jere alisema mafunzo hayo yamehuhduriwa na washiriki 92 wa aina na madaraja mbalimbali kutoka Kanda ya Ziwa na mikoa mingine nchini.

Alisema mafunzo hayo ya usimamizi wa fedha yalilenga kuwasaidia makandarasi kuwa na uelewa wa usimamizi wa rasilimali fedha hususan taarifa za mizania au balance sheet.

Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Injinia Consolata Ngimbwa akiwa kwenye picha ya pamoja na makandarasi wa mikoa mbalimbali mara baada ya kufunga mafunzo ya siku tatu kuhusu usimamizi wa fedha na kodi iliyofanyika mkoani Mwanza.

Alisema washiriki wa mafunzo hayo wamejifunza masuala ya kodi hususan namna nzuri ya kutunza kumbukumbu ili kuepuka mkodi zisizostahili au faini kama adhabu kwa kukiuka misingi muhimu ya uandaji wa mahesabu ya fedha za kampuni.

Injinia Jere alisema mafunzo hayo ni endelevu na mengine yanatarajiwa kufanyika kwa nyakati tofauti kwenye mikoa ya Iringa, Dar es Salaam na  Dodoma.

Alisema mafunzo hayo yanafanyika lengo ikiwa ni kuwajengea uwezo makandarazi wazalendo kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi ambayo sasa hivi inafanywa na kampuni za kigeni.

Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Injinia Consolata Ngimbwa akizungumza na maofisa wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) mara baada ya kufunga mafunzo ya siku tatu ya usimamizi wa fedha na kodi kwa makandarasi wazalendo.

Habari Kubwa