CRDB Mtwara yawashauri wanawake kufungua akaunti ya malkia

10Oct 2021
Abdallah Khamis
Mtwara
Nipashe Jumapili
CRDB Mtwara yawashauri wanawake kufungua akaunti ya malkia

​​​​​​​MENEJA Biashara wa Benki ya CRDB tawi la Mtwara Herieth Rwechungura, amewashauri wanawake mkoani humo kufungua akaunti ya malkia kwa ajili ya kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima hali inayowafanya washindwe kufikia malengo yao kwa wakati.

Zaiko kanjobe Meneja wa CRDB tawi la Mtwara.

Akizungumza na Nipashe mkoani humo, Rwechungura amesema uzoefu unaonyesha kuwa wanawake wengi wanashindwa kufikia malengo kutokana na kuwa wasimamizi wakuu wa familia zao hasa pale zinazojitokeza changamoto zinazohitaji matumizi ya fedha.

Mbali na wanawake kutumia akiba zao kwenye majukumu ya kifamilia yanayopaswa kufanywa na wanaume, Rwechungura ameeleza kuwa sababu nyingine ya kushindwa kufikia malengo ni pamoja na kuwa na matumizi yasiyo na mpangilio pale wanapokutana na vitu vizuri visivyokuwa katika bajeti ya wakati huo.

"Sisi CRDB tuna akaunti ya Malkia na walengwa ni wanawake wenye umri kuanzia miaka 18, ni sawa sawa na kibubu au ile michezo wanayocheza wakiwa na malengo maalumu, sema kwetu watakuwa katika utaratibu utakaowawezesha kufikia malengo hayo kwa wakati" amesema Rwechungura.

Ameongeza kuwa mwanamke yeyote anayefungua akaunti ya malkia baada ya mwaka ana uhuru wa kuendelea nayo au kukivunja kulingana na malengo aliyojiwekea Meneja wa CRDB tawi la Mtwara Zaiko Kanjobe, amesema akaunti ya Malkia imekuwepo kwa zaidi ya miaaka saba na kwa sasa wameshusha kianzio cha kufungulia akaunti kutoka shilingi 50,000 hadi 5,000 pasipo kuweka masharti.

Ameeleza kuwa faida anayopata mteja wa malkia akaunti ni pamoja kupata riba ya asilimia 1.5 kwa mkopo wa kuanzi sh.100,000 hadi sh milioni 4 na asilimia 2 kwa mkopo wa kuanzia sh milioni 5 hadi 10 na zaidi ya kiwango hicho riba yake ni asilimia 2.5 kwa mwaka.

"Hadi sasa tumefungua matawi 150 kwa tawi la Mtwara pekea yake ambapo tunaweza kuwakopesha malkia hawa kwa asilimia 14 kwa mwaka kutoka katika mkopo wa ujasiriamali, ambapo kwa wasiokuwa malkia mkopo huo wangekopeshwa kwa asilimia 20" amesema.

Ameongeza kuwa benki hiyo imejiwekea lengo la asilimia 80 ya wakopaji kuwa wananchi wa kawaida wajasiriamali na kuwataka wanawake kutumia fursa hiyo ya kupata mikopo.