CRDB yapongezwa kuwajali wazawa

08Nov 2019
Cynthia Mwilolezi
Arusha
Nipashe
CRDB yapongezwa kuwajali wazawa

MKUU wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuwapa nafasi ya uongozi wa juu katika benki hiyo Watanzania, tofauti na benki zingine.

MKUU wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, picha mtandao

Aliyasema hayo jana jijini alipofungua kongamano la 'Pamoja Nawe Kukuza Uchumi', lililokutanisha wadau wa benki hiyo Kanda ya Kaskazini.

Alisema benki hiyo imekuwa mstari wa mbele kuonyesha Watanzania wanaweza katika masuala ya uongozi.

"Benki hii imeonyesha njia benki zingine zinazotoa nafasi hizo kwa raia wa kigeni kwa kuwapa nafasi wazawa katika nafasi kubwa na wameonyesha wanaweza sababu benki imepiga hatua kila nyanja na inazidi kukua," alisifu.

Gambo alisema CRDB wametambua umuhimu wa kutumia vipaji vya wazawa katika kutekeleza miradi ya maendeleo na kuiendesha benki hiyo.

Alisema wanachofanya CRDB ni kuendeleza falsafa ya Rais John Magufuli ya kusaidia wananchi wanyonge kwa kuanza kutoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo bila masharti magumu na kutoa kipaumbele kwa wazawa.

Mkurugenzi wa Wateja wa Kati na Wadogo wa benki hiyo, Boma Raballa, alisema wameamua kutoa semina kwa wateja wao toka Kanda ya Kaskazini ili wafahamu fursa zilizopo benki na kuzitumia kuboresha biashara zao.

Alisema benki hiyo kwa sasa imejipanga kuinua Watanzania kwa kutoa mikopo yenye riba nafuu na isiyo na riba kwa wajasiriamali wenye vitambulisho vya Rais Magufuli.

"Sisi CRDB tumeona tuwezeshe wateja wetu katika kuwainua kwenye mitaji yao ya biashara kutokana na kutufanikisha kupata maendeleo katika benki yetu," alisema.

Alitaja baadhi ya mafanikio waliyonayo kuwa ni kufungua mashine za kielektroniki za ATM 550 na kufungua matawi 266 Tanzania nzima.

Habari Kubwa