CRDB yatoa chakula cha Eid kwa watoto yatima

23May 2020
Neema Hussein
Katavi
Nipashe
CRDB yatoa chakula cha Eid kwa watoto yatima

BENKI ya CRDB tawi la Mpanda mkoani Katavi, Iimetoa msaada wa chakula kwa watoto yatima wa dini ya Kiislam wanaoishi kwenye Manispaa ya Mpanda kwaajili ya Sikukuu ya Eid.

Akikabidhi msaada huo jana kwa Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Meneja wa CRDB tawi hilo, Hamad Masoud, alisema watoto hao wana haki ya kufurahia sikukuu kama walivyo watoto wengine ambao wana wazazi wao.

Masoud aliwataka watoto hao kutokujiona hawana thamani katika dunia, na kuwataka wasome kwa bidii huku wakiondoa fikra hizo kwa kuwa kuna watu wana historia kubwa katika maisha yao na sasa ni watu wakubwa hapa duniani.

"Yawezekana ukawa unajiona upo katika mazingira magumu sana, yawezekana ukawa umekata tamaa sana, yawezekana ukajiona wewe hapa duniani hufai, lakini mimi niwatie moyo na mjuwe kuwa Mwenyezi Mungu ndiyo mtoa riziki," alisema Masoud.

Shekhe Mkuu wa Mkoa, Mashaka Kakulukulu, aliishukuru benki hiyo kwa kufanya tukio hilo muhimu la kuwakusanya watoto na kuwapa zawadi kwaajili ya Eid kama vitabu vya dini vinavyo elekeza.

Alisema hiyo iwe ni ishara kwa Taasisi zingine au mtu mmoja mmoja kuiga mfano huo uliofanywa na benki hiyo na kujua kwamba wanao wajibu wa kuwalea watoto hao kwa sababu hawakupenda kuondokewa na wazazi wao.

Watoto waliopewa msaada huo pia walitoa shukrani zao kwa benki hiyo na uongozi wa Bakwata kwa kuwajali na kuwakumbuka katika kipindi cha Sikukuu ya Eid na kuomba waendelee kuwasaidia na kuwalea katika mazingira ya dini.

Habari Kubwa