Dar wafagilia katazo mifuko ya plastiki

12Jun 2019
Enock Charles
Dar es Salaam
Nipashe
Dar wafagilia katazo mifuko ya plastiki

SIKU kadhaa baada ya kuanza  kwa utekelezaji wa katazo la utumiaji, usambazaji na utengenezaji wa mifuko ya plastiki, maisha yamerudi katika hali ya kawaida, huku mifuko mbadala ikichukua nafasi.

Wakazi kadhaa wa Jiji la Dar es Salaam wamefunguka kuelekeza kwao kufurahishwa na utekelezaji wa katazo hilo.

Katika mahojiano na wadau mbalimbali katika jiji hilo wakiwamo wasambazaji na watumiaji wa mifuko mbadala wameeleza kufurahishwa na utekelezaji huo uliofanyika bila matumizi ya nguvu.

Mfanyabiashara wa mifuko mbadala awali alikuwa muuzaji wa mifuko ya plastiki eneo la Yombo Vituka, Yunus Mwakikuti, alipongeza hatua iliyochukuliwa na serikali na kuwa  hali imerejea vizuri na uhitaji wa mifuko hiyo katika kubebea bidhaa ni wa uhakika.

“Naipongeza serikali kwa uamuzi huo mzuri kwa kulinda mazingira na afya za watu wake. Napongeza pia mamlaka zilizoshiriki kuhakikisha katazo hili linatekelezeka pasipo kutumia nguvu  zaidi ya kuelimisha watu juu ya athari za moja kwa moja zinazoonekana katika jamii kutokana na matumizi ya mifuko ya plastiki,” alisema Mwakikuti.

Zakia Abdalah, mfanyabiashara soko la  Mbagala Rangi Tatu, alisema katazo la serikali limekuwa na maana kubwa kimazingira kwani mifuko ya plastiki ingeachwa kutumika ingeleta madhara makubwa kwa mazingira na afya.

“Siku ya kwanza ilikuwa na usumbufu mkubwa kutokana na mazoea ya watu kutumia mifuko ya plastiki, lakini kwa sasa mambo yanakwenda vizuri tumeshazoea kutumia mifuko mbadala kutokana na uimara wake na unaweza kuitumia kwa muda mrefu kulingana na matumizi yako tofauti na mifuko ya plastiki,” alisema Abdalah.

Alisema mamlaka husika ziendelee kutoa elimu kuhakikisha wanawajengea uwezo wananchi juu ya umuhimu wa utunzaji wa mazingira na faida zake kwa jamii iliyopo sasa na vizazi vijavyo kuhusu faida ya utunzaji wa mazingira.

Akizungumza hivi karibuni, Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifidhi wa Mazingira (NEMC), Dk. Samuel Gwamaka, alisema baraza lake litaendelea kutoa elimu na kuhakikisha ufuatiliaji na usimamizi wa sheria za mazingira unafuatwa kama inavyoelekezwa.

“Hakuna nguvu iliyotumika zaidi ya kutoa elimu kwa wananchi juu ya madhara ya mifuko ya plastiki katika mazingira,  hivyo tutaendelea kuhakikisha sheria na kanuni za usimamizi wa mazingira zinafuatwa kikamilifu ili kulinda mazingira ya  nchi yetu,” alisema Dk. Gwamaka.

Dk. Gwamaka alisema NEMC imewataka wataalamu katika mikoa yote hapa nchini kuhakikisha elimu inatolewa kwa wananchi na utekelezaji wa katazo linaendelea kutekelezwa ili kunusuru taifa kuingia katika athari za kimazingira kutokana na matumizi makubwa ya mifuko ya plastiki.

Habari Kubwa