Dawa za kulevya zapenya magerezani Zanzibar

19Mar 2017
Mwinyi Sadallah
Nipashe Jumapili
Dawa za kulevya zapenya magerezani Zanzibar

TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imesema kuna udhibiti mdogo wa dawa za kulevya kwa wafungwa na mahabusu visiwani hapa.

heroin.

Kauli hiyo ilitolewa juzi na Kamishina Mkazi wa tume hiyo, Mohamed Khamis Hamad, alipokuwa akizungumzia vita dhidi ya dawa za kulevya visiwani Zanzibar.

Alisema sigara, 'unga' na bangi zinawafikia wafungwa na mahabusu katika magereza kutokana na udhibiti kuwa mdogo.

“Uchunguzi tuliofanya kuna wafungwa au mahabusu wanaingia na vitu wakati mwingine hadi pesa wakificha katika sehemu za siri na kuzitumia kununua 'unga' (dawa za kulevya) na sigara,”alisema.

Hamad alisema tatizo hilo linaweza kuondolewa iwapo mamlaka zenye dhamana zitaongeza ukaguzi na kufanyika kwa umakini na uadilifu.

"Vita dhidi ya dawa za kulevya inayoendelea itafanikiwa iwapo wananchi watakuwa tayari kusadia kufichua kwa siri watu wanaouza katika mitaa yao, lakini mamlaka zenye dhamana lazima ziwe tayari kulinda siri."

"Juhudi zinazoendelea kufanyika zinaweza kufanikiwa kuondoa kabisa tatizo la biashara haramu ya dawa za kulevya, lakini uchunguzi wa kina lazima ufanyike kabla ya watuhumiwa kukamatwa ili kuepusha kukamatwa watu wasiokuwa na hatia," alisema.

Habari Kubwa