DC aagiza wajasiriamali wenye mafunzo wapewe mikopo

19Mar 2019
Nebart Msokwa
Mbozi
Nipashe
DC aagiza wajasiriamali wenye mafunzo wapewe mikopo

MKUU wa Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, John Palingo, ameiagiza ofisi ya Ofisa Maendeleo ya Jamii wa wilaya hiyo kuvipa kipaumbele wakati wa utoaji wa mikopo ya halmashauri kwa vikundi vya wajasiriamali vilivyopatiwa mafunzo maalumu ya uendeshaji wa biashara.

Alitoa agizo hilo mwishoni mwa wiki alipokuwa mgeni rasmi kwenye Sherehe za Mradi wa Uwezeshaji Biashara (Sirolli) unaotekelezwa na Shirika la Heifer International kwa kushirikiana na Taasisi ya Sirolli ya nchini Marekani katika Wilaya ya Mbozi.

Alisema wananchi hao wamepata elimu ambayo itawasaidia kuendesha biashara zao kwa ufanisi na kuwa na uwezo wa kurejesha mikopo hiyo kwa wakati, hivyo ni vema wapewe kipaumbele kuliko wale ambao hawana mafunzo hayo.

Alilipongeza Shirika la Heifer kwa kufadhili mradi huo kwa madai kuwa utakuwa na manufaa kwa wananchi hao hasa wajasiriamali wadogo kwa madai kuwa watakuwa na uwezo wa kuendesha biashara zao kisasa na kuweza kukua kiuchumi.

“Elimu hii ni muhimu sana hasa wakati huu ambapo serikali ya awamu ya tano inasisitiza uchumi wa viwanda, sasa hawa wenzetu wametoa elimu ya bure kabisa kwa hawa wajasiriamali, sasa ni vema na sisi tukawapa kipaumbele kwenye utoaji wa mikopo,” alisema Palingo.

Alisisitiza kuwa baada ya kukagua baadhi ya bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali walionufaika na mradi huo wanazalisha bidhaa nzuri na wanaendesha biashara zao kwa mbinu za kisasa zaidi.

Aliwashauri baadhi ya wazalishaji hao hasa wanaozalisha vyakula kuhakikisha wanaziona mamlaka zinazohusika ikiwamo Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Shirika la Viwango Tanzania TBS, ili zithibitishe ubora wa bidhaa hizo.

Baadhi ya wajasiriamali walionufaika na mradi huo wa Sirolli walisema wamepata manufaa makubwa kutokana na mradi huo kwa kujifunza mbinu za uendeshaji wa biashara zao.

Habari Kubwa