DC ajitwisha zigo kero umeme viwandani

22Jul 2021
Shaban Njia
Kahama
Nipashe
DC ajitwisha zigo kero umeme viwandani

MKUU wa Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, Festo Kiswaga, imelipa miezi sita Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha ndani ya miezi hiyo kunakuwa na umeme wa uhakika katika mji wa Kahama ili wawekezaji wajenge viwanda kwa wakati.

Kiswaga alibainisha hayo alipokuwa akizungumza na wafanyabiashara, TRA, Mamlaka za maji, Taasisi za kifedha na kamati ya ulinzi na usalama wakati akitambulisha maonyesho ya kimataifa ya biashara na uwekezaji yanayotarajia kufanyika katika Manispaa ya Kahama, kwa lengo la kutangaza biashara zao.
 
Alisema ofisi yake imekuwa ikipata malalamiko mengi kutoka kwa wananchi na wawekezaji juu ya kukatika kwa umeme mara kwa mara na kusababisha wawekezaji kushindwa kujenga viwanda vya uchakataji wa mazao na kuwataka kutatua changamoto hiyo mara moja.
 
“Nimepata malalamiko mengi tangu nimefika hapa, nishati ya umeme katika Wilaya ya Kahama ni shida, hali ambayo inafanya wawekezaji wengi kushindwa kuwekeza katika Manispaa hii…ninatoa miezi sita tatizo hili liwe limetatuliwa haraka,” alisema Kiswaga. 
 
Kiswaga alisema ukuaji wa mji wa Kahama kwa sasa ni mkubwa na lazima kuwe na viwanda vya kutosha ili wananchi wapate ajira kwa kufanya kazi na kukidhi mahitaji yao.
 
Nae Mwasiti Bajora, Mkazi wa Kata ya Majenga, alimpongeza mkuu wa wilaya kwa kuliona hilo, na kwamba yeye ni mjasiriamali ndogo anayesaga karanga, lakini umeme umekuwa ukikatika na kukwamisha shuhuli zake, na kwamba badala ya kukua, anazidi kudidimia kwa kukosa wateja.
 
Mjasiriamali Baraka Kasindi alisema wilaya hiyo ina maeneo makubwa ya uwekezaji wa wawekezaji wa ndani na nje, lakini wanashindwa kujitokeza kwa sababu hakuna umeme wa uhakika hasa katika Halmashauri za Msalala na Ushetu, ambapo ndipo kwenye maeneo makubwa.

Habari Kubwa