DC apiga ‘stop’ kilimo Mto Simiyu

03Nov 2017
Happy Severine
Nipashe
DC apiga ‘stop’ kilimo Mto Simiyu

MKUU wa Wilaya ya Itilima, Benson Kilangi, amepiga marufu wananchi  wanaopakana na Mto Simiyu kuacha mara moja shughuli za kilimo, ufugaji na ukataji wa miti kando kando ya mto huo.

Kilangi amechukua uamuzi huo kutokana na kuendelea kukithiri kwa kilimo na ukataji miti ovyo katika eneo la mita 60 za mto huo.

Alisema hayo juzi wakati wa hafla ya kukabidhi trekta kwa kikundi cha kilimo cha Madilana kilichoko katika kijiji cha Madilana, Kata ya Mhunze. Kikundi hicho kinaundwa na wananchi wenye mashamba yanayopakana na mto huo.

Kabla ya kukabidhi trekta hilo, Kilangi alitembelea na kuangalia eneo la mto lilivyoharibiwa hasa ukataji miti na kueleza kuwa uharibifu huo umekuwa mkubwa.

“Uharibifu ambao nimeuona huko unafanyika wakati viongozi wa vijiji, vitongoji na kata wapo na hawachukui hatua yoyote. Huu mto ni chanzo cha maji Ziwa Victoria, hivyo ni lazima kulindwa,” alisema.

Alionya kuwa mtu yeyote atakayekutwa ndani ya mto huo akifanya shughuli yoyote, atakamatwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria huku akitoa maagizo kwa viongozi wa vijiji kusimamia jambo hilo.

Ofisa Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima, Kelisa Wambura, alisema kwa muda mrefu wananchi wanaopakana na mto huo wamepewa taarifa za kuacha mara moja shughuli za kilimo lakini wamekuwa wakikaidi.

“Kuna wengine wanataka tuwapatie muda tena ili mazao yao yakomae wavune. Tumetoa taarifa mapema tukiwataka kusitishwa shughuli hizo, lakini wamegoma. Kwa hiyo msako ukianza tutawakama hata ambao wameanza kulima,” alisema Wambura.