DC asaka fursa ajira kwa vijana wa Siha

29Jun 2022
Anjela Mhando
Siha
Nipashe
DC asaka fursa ajira kwa vijana wa Siha

MKUU wa Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, Thomas Apson, amesema atakutana na kampuni zinazoendesha biashara ya utalii katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro ili kujadiliana nao namna yanavyoweza kutumia nguvu kazi ya vijana iliyopo wilayani humo.

Siha ni wilaya pekee mkoani Kilimanjaro yenye malango mawili ya kupokea watalii wanaopanda Mlima Kilimanjaro ambayo ni Lemosho na Lendrosi.

Apson alibainisha mpango huo juzi alipozindua mbio za West Kilimanjaro Marathon katika eneo la Simba Farm, West Kilimanjaro.

“Katika wilaya yetu kuna mageti mawili, lakini wazawa wa maeneo haya ya Siha wamekuwa hawanufaiki japo wana uwezo wa kutosha na nguvu za kutosha kupandisha watalii mlimani.

“Ni kweli wamekuwa hawapati fursa ya kupanda na wageni, kuwaonyesha Mlima Kilimanjaro, lakini cha ajabu na kinachosikitisha sana, kampuni za mkoa jirani wa Arusha zinakuja na watu wao. Nimesema hapana, huku ni kuwanyima wenyeji fursa hiyo," alisisitiza.

Alisema kutokana na hilo, ameamua atakutana na kampuni hizo kuwaomba wanapopita katika eneo la Siha, watenge nafasi chache kwa ajili ya wananchi wa Siha.

Meneja wa Shamba la Miti la Wakala wa Misitu Tanzania (TFS- West Kilimanjaro),Yahaya Masawanga, alisema lengo la kuanzisha mbio hizo ni kuhamasisha vivutio mbalimbali vya utalii vilivyomo wilayani humo.

"Tunataka kupitia mbio hizi, wageni waone mawe ya asili ambayo Wachaga wakifika eneo hili, wanayaita kaniitieni. Kihistoria wamesema yanapatanisha wapenzi ambao kama wakigombana, wanayatumia kupatana,” alisisitiza.

Habari Kubwa