DC ashtukia hujuma kwenye pembejeo

27Sep 2021
Yasmine Protace
Mkuranga
Nipashe
DC ashtukia hujuma kwenye pembejeo

MKUU wa Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, Khadija Ally, ameiomba serikali iruhusu kila wilaya ijitafutie pembejeo yenyewe na kuachana na wasambazaji.

Alisema wasambaji hawafikishi pembejeo kwa wakati na hali hiyo inachangia kuwapo kwa kikwazo kwa wakulima wa korosho.

Khadija aliyasema hayo katika kikao cha wadau wa korosho katika Mkoa wa Pwani ambapo mwenyekiti wa kikao, alikuwa Mkuu wa Mkoa huo, Abubakari Kunenge.

Khadija alisema ucheleweshwaji wa pembejeo una changamoto kutokana na pembejeo kutokufika kwa wakati.

"Ikiwezekana kila wilaya isimamie masuala ya pembejeo ili ijitafutie yenyewe," alisema na kuongeza kuwa katika usambazaji pembejeo kuna hujuma kubwa ambazo ni za makusudi.

Alisema pembejeo wakati wa msimu zinakuja kidogo na hizifiki kwa wakati, lakini msimu wa korosho ikiisha ndipo zinapoonekana zikiwa nyingi.

Kwa upande wake, Kunenge naye alionyesha kushangazwa na taarifa za pembejeo na mbolea katika taarifa zilizochapishwa na kugawiwa kwa wadau wa korosho kuzisoma.

Alisema taarifa hizo zinaleta utata kutokana na pembejeo na mbolea kutolewa kwa wakulima mmkoa wa Pwani.

"Mbona hamjaonyesha katika taarifa yenu pembejeo na mbolea kiasi kilichotolewa ikiwamo na idadi ya mikorosho iliyopo Pwani," alisema.

Alisema taarifa hiyo, inatakiwa kuwa imejitoshleza na isije kuleta shida na kwamba inatakiwa ionyesha idadi ya mikorosho iliyopo Pwani na pembejeo pamoja na mbolea zilikuwa kiasi gani na mgao wake ulipelekwaje kwa halmashauri zote.

Habari Kubwa