DC Kilolo ajitosa kuinusuru Saccos

20Jan 2019
George Tarimo
Ilula
Nipashe Jumapili
DC Kilolo ajitosa kuinusuru Saccos

MKUU wa Wilaya ya Kilolo, Asia Abdallah, ameongoza mkutano maalumu kati yake na na wadaiwa sugu wa chama cha ushirika cha akiba na mikopo (Saccos) cha Mazombe, kilichoko katika mji mdogo wa Ilula.

MKUU wa Wilaya ya Kilolo, Asia Abdallah.

Mkutano huo uliofanyika juzi, ulikuwa mahsusi kwa ajili ya kujadili jinsi ya kuwabana na kulipa madeni wadaiwa hao ambayo ni zaidi ya Sh. milioni 354 ambazo wengi  wamekopa na kushindwa kurejesha kwa wakati.

Akizungumza katika mkutano huo, mkuu huyo wa wilaya alisema tatizo kubwa wananchi wengi wanakopa pasipokuwa na mipango ndiyo maana wengi wanashindwa kurejesha.

“Wengi wenu mnakopa bila kuwa na mipango, mnakopa kwa ajili ya kununua madela, kuuza ulanzi na mambo mengine ambayo mwisho wa siku fedha zinaisha zote,” alisema Abdallah na kuongeza:

“Mmeanzisha taasisi hii kwa ajili yenu wenyewe, mkikopa halafu mkashindwa kurejesha maana yake mnaiua ninyi wenyewe wakati chama hiki kimeshakua na kutambulika kitaifa na kimataifa. Nikiwa msimamizi wa hiki chama sitakubali kinifie, nitapambana nanyi ili kila mkopaji alipe kwa wakati deni lake,” alisema.

Awali, akisoma taarifa ya madeni ya chama hicho,  Mwenyekiti wa Bodi ya Mazombe Saccos, Yohana Mwemutsi, alisema hadi Desemba 31, mwaka jana, madeni sugu yalikuwa Sh. 354, 001, 630 kati ya mikopo yote iliyoko nje ambayo ni Sh.  998,013,797 sawa na asilimia 35.4 ya mikopo yote.

Mwemutsi alisema katika mkutano mkuu uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana, lilitolewa azimio la kuomba Mkuu wa Wilaya kukutana na wadaiwa sugu ili kutoa msimamo wa serikali kuhusu madeni ambayo yamekuwa hayalipiki.

Katika hotuba yake aliyoitoa katika mkutano mkuu wa chama hicho mwishoni mwa mwaka jana, Abdallah aliagiza watu wote ambao hawajarejesha mikopo kwa wakati wachukuliwe hatua kali za kisheria kwa kuwa ushirika ulio imara hautawafumbia macho watu wenye nia ovu ya kudidimiza maendeleo ya ushirika nchini.

Hata hivyo, baada ya mkuu huyo kutoa agizo hilo, wadaiwa hao walilipa Sh.  8,891,597.

Habari Kubwa