DC Odunga aonya hujuma ugawaji vitambulisho vya ujasiriamali

12Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Chemba
Nipashe
DC Odunga aonya hujuma ugawaji vitambulisho vya ujasiriamali

MKUU wa Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma Simon Odunga amewaonya wafanyabiashara wakubwa wanaojipenyeza kupata vitambulisho vya ujasiriamali huku akiwataka watendaji wa vijiji na kata kuwa waadilifu katika zoezi la kuwatambua.

MKUU wa Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma Simon Odunga

Agizo hilo limekuja baada ya kupata taarifa kuwa kuna baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wanataka kunufaika na fursa hiyo wakati wao sio walengwa.

Akitoa vitambulisho hivyo, Odunga alisema kamati ya uratibu ilizunguka katika kata zote za wilaya hiyo na kubaini wafanyabiashara hao kujipenyeza ili kupata vitambulisho hivyo.

“Nyie watendaji hakikisheni hivi vitambulisho vinagaiwa kwa uadilifu mkubwa, na nitaendelea kuwa sambamba kwenye hili zoezi kuhakikisha vinatolewa kwa wale wanaostahili,”alisema.

Alisema vitambulisho hivyo vinafaida kubwa kwa wajasiriamali hivyo ni vyema wakajitokeza kuchangamkia fursa hiyo.

“Tumetoa semina kwa watendaji wa vijiji na kata ili wasimamie zoezi hili na tukubaliane kwenye vigezo ili zoezi hili lisichakachuliwe,”alisisitiza.

Alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha zoezi la utambuzi na utoaji wa vitambulisho hivyo linafanyika kwa muda mfupi likamilike ndani ya wiki moja.

Awali akisoma taarifa ya utambuzi wa wajasiriamali hao, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chemba Dk.Semistatus Mashimba alisema wamebaini changamoto hiyo ya wafanyabiashara kujipenyeza katika orodha ya wajasiriamali wadogo ili kupata vitambulisho.

“Tulibaini udanganyifu ambapo baadhi ya wafanyabiashara wakubwa walikuwa wakijaribu kudanganya kiwango cha mauzo ya bidhaa zao kwamba kipo chini ya Sh.Milioni nne kwa mwaka wakati si kweli,”alisema.

Alisema kutokana na hali hiyo walifanya uhakiki na kuwatoa wale wote waliofanya udanganyifu huo.

Nao, baadhi ya wajasiriamali walimshukuru Rais John Magufuli kwa utoaji wa vitambulisho hivyo kwa kuwa walikuwa wakifanya kazi kwenye mazingira magumu.

Habari Kubwa