Dk. Mwinyi ahimiza kulinda, kuhifadhi Bahari ya Hindi

26May 2023
Rahma Suleiman
ZANZIBAR
Nipashe
Dk. Mwinyi ahimiza kulinda, kuhifadhi Bahari ya Hindi

RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema vipaumbele vya maendeleo ya Tanzania vinafungamana na Bahari ya Hindi hivyo ni vyema kuilinda na kuihifadhi bahari hiyo.

 

Aliyasema hayo wakati akifungua mkutano wa tisa wa mazungumzo ya Bahari ya Hindi uliofanyika visiwani Zanzibar, ambapo hotuba yake ilisomwa na Makamu wa Kwanza wa Rais, Othman Masoud Othman kwa niaba yake.

Alisema mabadiliko ya haraka ya kiuchumi yameathiriwa kwa kiasi kikubwa na mfumo ikolojia wa biashara ya baharini wa huduma za baharini, biashara na miundombinu ya bandari.

“Tumebarikiwa, hakika tumepewa zawadi ya Zanzibar kama paradiso ya utalii katika ukanda huu. Tunaendelea vyema katika kugusa na kutumia kwa uwajibikaji gesi asilia ya nje ya nchi na vyanzo vingine vya nishati,”alisema.

Dk. Mwinyi alisema Tanzania ni taifa linalochipukia katika adhma ya uvuvi wa bahari kuu na wakati huo huo kubadilisha maisha ya wavuvi na jamii za wafugaji wa samaki.

Aidha, alisema kuna haja ya kuimarisha uwezo na kuendeleza mihimili ya ulinzi kuelekea ufadhili wa rangi ya buluu na hali ya hewa ambayo inanufaisha jamii.

“Hii itakuwa ushindi kwa uchumi wa buluu, ustahimilivu wa bahari duniani, kukabiliana na hali ya hewa, usawa wa kijamii na malengo ya maendeleo endelevu”alisema.

Hata hivyo alisema uwezeshaji wa wanawake na ujumuishaji wa jinsia katika uuchumi wa buluu ni muhimu ili kuleta ufanisi wa uchumi jumuishi, unaojumuisha na wenye ushirikiano.

Naye Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Masoud Suleiman Makame alisema, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua ungwaji mkono na ahadi za IORA, kuelekea kuinua matarajio ya uchumi wa buluu.

“Sote tunakubali kwamba ili uchumi wa buluu ufanikiwe, tunahitaji kuunganisha vipaumbele vyetu vya maendeleo na uendelevu, ushirikishwaji wa kijamii, na ushiriki wa sekta ya kibinafsi, katika ajenda yetu ya maendeleo ya bahari”alisema Waziri huyo.

Aidha, alisema kujitolea kwa viongozi wa nchi Rais Samia na Rais Dk. Mwinyi kuelekea mazungumzo ya kikanda na kimataifa kuhusu uchumi wa buluu na utawala wa bahari, kumerejesha nafasi ya Tanzania miongoni mwa familia za mataifa, kwa kufuata diplomasia ya uchumi wa pande zote kwa manufaa ya watu wake wote.