Dodoma, Manispaa Iringa vinara ukusanyaji mapato

20Jan 2019
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe Jumapili
Dodoma, Manispaa Iringa vinara ukusanyaji mapato

HALMASHAURI Jiji la Dodoma na ile ya manispaa ya Iringa, zimeibuka kidedea katika makusanyo ya mapato katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha wa 2018/19.

Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, alisema jana jijini hapa alipokuwa akitoa taarifa juu ya makusanyo ya mapato kwa halmashauri katika kipindi cha Julai hadi Desemba, mwaka jana.

Alisema uchambuzi unaonesha kuwa, kati ya majiji sita yaliyoko nchini, Halmashuri ya Jiji la Dodoma inaongoza kwa kukusanya asilimia 59 ya makisio huku jiji la Tanga likishika nafasi ya mwisho katika kundi la majiji kwa kukusanya asilimia 33 ya makisio.

“Halmashauri ya Manispaa ya Iringa imeongoza katika kundi la manispaa kwa kukusanya asilimia 64 ya makisio huku Manispaa ya Lindi ikiwa ya mwisho katika kundi hili kwa kukusanya asilimia 20,” alisema.

Kwa upande wa halmashauri za miji, alisema Mji Geita imeongoza kwa kukusanya asilimia 84 na Mji Nanyamba imekuwa ya mwisho katika kundi hilo kwa kukusanya asilimia tisa.

Katika kundi la halmashauri za wilaya, Geita imeongoza kwa kukusanya asilimia 78 ya makisio wakati Nanyumbu imekuwa ya mwisho kwa kukusanya asilimia sita tu.

Jafo alisema halmashauri iliyoongoza kwa kukusanya mapato ya ndani kwa wingi ni  Jiji la Dodoma ambayo katika kipindi cha Julai – Desemba, mwaka jana, ilikusanya Sh. bilioni 40.12.

“Halmashauri iliyokusanya kiasi kidogo cha mapato ya ndani ni Halmashauri ya Wilaya ya Momba iliyokusanya Sh. Milioni 105.04.

Jafo pia alisema halmashauri 64 zimekusanya zaidi ya Sh. bilioni moja katika kipindi hicho.

MAKUSANYO KIMKOA

Kimkoa, Jafo alisema mkoa wa Dar es Salaam umeongoza kwa kukusanya Sh. bilioni 77.04, ukifuatiwa na Dodoma ambao umekusanya Sh. bilioni 44.8 huku wakati Katavi ikiwa ya mwisho baada ya kukusanya Sh. bilioni 2.4.

“Mkoa wa Geita umeibuka kinara kwa ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kipindi cha nusu mwaka kwa kukusanya asilimia 56.4 ya makisio ya mwaka wa fedha 2018/19 ukifuatiwa kwa karibu na Dodoma uliokusanya asilimia 55.9 huku mkoa wa  mwisho kwa kigezo hicho ni Mtwara ambao umekusanya asilimia 15 ya makisio yake ya mwaka,”alisema.

Changamoto

 

Alitaja changamoto saba zilizozikabili halmashauri katika ukusanyaji wa mapato ya ndani katika kipindi cha Julai - Desemba katika mwaka wa fedha 2018/19.

“Baadhi ya wanunuzi kuchelewa kulipa ushuru kwa halmashauri na kusababisha halmashauri hizo kuonekana zimekusanya chini ya kiwango na baadhi ya Halmashauri kutegemea zaidi chanzo kimoja na kushindwa kukusanya kutoka kwenye chanzo hicho ni changamoto zilizojitokeza katika mchakato huu hata kusababisha halmashauri hizo kushindwa kujiendesha,” alisema.

Changamoto zingine ni matumizi mabovu ya mifumo ya kukusanya mapato kwa njia za kielekroniki kwa baadhi ya halmashauri, baadhi ya halmashauri kutumia takwimu za makisio zisizo na uhalisia na kushindwa kuweka mikakati madhubuti ya kukusanya mapato kutoka kwenye vyanzo vipya vinavyobuniwa.

Habari Kubwa