DTB yamwaga bil. 275/- kipato cha chini

03Aug 2017
Beatrice Shayo
Dar es salaam
Nipashe
DTB yamwaga bil. 275/- kipato cha chini

BENKI ya Diamond Trust (DTB) imesema katika kuhakikisha inasaidia wananchi wenye kipato cha chini, imetoa mkopo wenye thamani ya Sh. bilioni 275 kwa ajili ya wajasiriamali wadogo na wale wa kipato cha kati mpaka sasa.

Mkurugenzi Mtendaji wa DTB, Viju Cherian.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa DTB, Viju Cherian, wakati wa uzinduzi wa tawi jipya la benki hiyo la Barabara ya Uhuru, katika eneo la Kariakoo, Manispaa ya Ilala na kuongeza idadi ya matawi kufikia 28 nchi nzima.

Alisema benki hiyo imejikita katika kuhakikisha inawainua wajasiriamali wadogo na wenye kipato cha kati ili waweze kukua kiuchumi na kuondokana katika hali ya umaskini.

"Tumejikita kuwawezesha wajasiriamali," alisema. Cheria na "huu ni mkakati wetu na kiasi cha Sh. bilioni 275 sawa na asilimia 43 ya jumla ya mikopo ya benki yetu imeenda kwa wajasiriamali."

Aidha, Cherian alisema benki hiyo inajivunia katika kipindi cha miaka 71 ya kutoa huduma za kifedha kwa Watanzania kutokana na kuendelea kukua kibiashara na kiutendaji.

"Ufunguzi wa tawi hili la Uhuru ni moja ya hatua katika kuongeza huduma kwa wananchi ili waweze kuzipata kwa wakati," alisema. "Tuna mpango wa kufungua matawi mengine mawili ndani ya miezi 12 ijayo ili kukuza mtandao wetu wa matawi ili yafike 30."

Mmoja wa wafanyakazi wa benki hiyo, Sylvesta Bahati alisema kufunguliwa kwa tawi hilo kumewalenga wafanyabiashara wa Kariakooo ili waweze kupata huduma kwa wakati.

Alisema kuna kampeni ya 'Chakarika Akaunti' ambayo ni kwa ajili ya wafanyabiashara, hivyo wanahimizwa kuacha kutumia akaunti binafsi katika kuendesha shughuli zao.

"Ni vizuri wafanyabiashara wakafika katika matawi yetu ya DTB na kujipatia akaunti maalumu ya biashara kuliko kuchanganya akaunti binafsi na biashara," alisema Bahati.

Habari Kubwa