EFL yaanzisha mwezi huduma kwa wateja

14Oct 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
EFL yaanzisha mwezi huduma kwa wateja

KAMPUNI ya Enterprise Finance Limited (EFL), inayojishughulisha na huduma za fedha kwa wafanyabiashara na wafanyakazi, imezindua utaratibu wa kusherehekea mwezi wa huduma kwa wateja itakayofanyika Oktoba kila mwaka.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni ya Enterprise Finance Ltd (EFL), Prof. Goodluck Urasa (kushoto), akizungumza na wafanyakazi, jijini Arusha hivi karibuni, wakati wa uzinduzi wa utaratibu wa kusherehekea mwezi wa huduma kwa wateja wa kampuni hiyo, ambao uadhimishwa mwezi Oktoba kila mwaka. PICHA: MPIGAPICHA WETU

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Prof. Goodluck Urassa, utaratibu huo ni mpya na kwamba una lengo la kukamilisha shughuli mbalimbali ilizokusudia kufanya katika kuboresha huduma zake.

Lengo lingine ni kuboresha huduma kwa wateja kila siku, utaratibu utakaowezesha menejimenti na wafanyakazi kushirikiana kujenga utamaduni wa kuwahudumia wateja kwa weledi na ubora wa hali ya juu kwa mwezi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa EFL, Jacqueline Lujuo, alisema  EFL imejipanga kuboresha uhusiano na wateja kwa kutoa huduma za ziada na kwamba wameweka utaratibu wa kuwatembelea kujua mahitaji yao, kusikiliza changamoto, kutoa ushauri wa kibiashara kwa wateja na jamii, kutoa mafunzo ya ujasiriamali na usimamizi wa fedha kwa wajasiriamali wanaopenda kushiriki na kujenga uwezo wa wafanyakazi kuwahudumia wateja kwa ufanisi.

Pia alisema EFL itajihusisha na shughuli za kijamii ikiwa ni pamoja na kuandaa michezo mbalimbali kati yake na taasisi nyingine ili kuchangia katika kuimarisha afya za wafanyakazi, wateja na jamii.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, taasisi hiyo imekusudia kuhakikisha kila mteja au mjasiriamali anayehudumiwa anajengewa uwezo wa kukua kibiashara.

“Mafunzo haya yalilenga kuwawezesha washiriki kuibua fursa za kijasiriamali, kusimamia biashara, kusimamia fedha na kujenga tabia ya uwajibikaji pia tunaendelea kutoa ushauri na mafunzo zaidi kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari na imeishauri jamii kufuatilia vipindi vyake,” alifafanua.

Mmoja wa washirikia hao, Getruda Laizer, aliishukuru taasisi hiyo kwa mikopo nafuu iliyowawezesha kukuza biashara zao.

Naye Godfrey Massawe ambaye ni mkandarasi, alisema EFL imekuwa mkombozi wao kwa kuwapatia mikopo kwa wakati kwa ajili ya kutekeleza miradi.

Meneja wa EFL, Tawi la Arusha, Hekima Adam, alisema kampuni imejipanga kuwafikia wafanyakazi na wajasiriamali wote Kanda ya Kaskazini.