Ekari 500 zatengwa ujenzi wa mtambo kuchakata madini

02Sep 2017
John Ngunge
Nipashe
Ekari 500 zatengwa ujenzi wa mtambo kuchakata madini

EKARI 500 zimetengwa katika Mamlaka ya Mji mdogo wa Mirerani, kwa ajili ya kujenga mtambo wa kuchakata madini.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dk. Joel Bendera.

Tayari gharama ya ununuzi wa eneo hilo ambalo litajengwa pia kituo cha kuuzia madini (EPZ), umeshafanyika ikiwa pamoja na kuwalipa fidia wakazi waliokuwa wakiishi humo pamoja na kujenga viwanda vingine vitakavyotoa fursa ya ajira kwa vijana na wanawake.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dk. Joel Bendera, alisema hayo juzi wakati akizungumza na wafanyabiashara wa mkoa huo ambao ni wanachama wa Chama cha Wafanyabiashara, Wakulima na Wenye Wiwanda (TCCIA).

Alisema kukamilika kwa malengo hayo kutainua uchumi wa mkoa huo kwa kiasi kikubwa.

Alitaja baadhi ya viwanda vinavyotarajiwa kujengwa kuwa ni cha mafuta ya kula na alizeti.

Aliwataka wafanyabiashara hao kujitathmini na kuangalia changamoto zinazowakabili na jinsi ya kupanua uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla.

"Tumepata kiwanja, sasa biashara ya madini itafanyika Manyara na siyo kwenda Arusha tena.

“Madini yapo mkoani kwetu, lakini biashara zinafanyika Arusha,

EPZ ingejengwa hapa na tumeshapata eneo, biashara hiyo itafanyika wilayani Simanjiro mji mdogo wa Mirerani na duniani kote watakaohitaji madini ya Tanzanite lazima waje Manyara," alisema.

Makamu wa Rais TCCIA Tanzania, Octavian Mshiu, akizungumza kwa niaba ya Rais wa vyama vya TCCIA alimuomba Mkuu wa Mkoa wa Manyara, kupunguza bei za viwanja vinavyoombwa kwa ajili ya kuanzisha viwanda na kuhakikisha halmashauri husika inatangaza viwanja hivyo ili nchi nzima ijue na waweze kununua.

Alisema mkoa huo unahitaji kuwa na kiwanda cha usindikaji wa chakula kutokana na wakazi wake wengi kuwa ni wakulima.

Habari Kubwa