Elimu vijana uchumi wa viwanda

14May 2018
Rahma Suleiman
ZANZIBAR
Nipashe
Elimu vijana uchumi wa viwanda

WAZIRI wa Viwanda na Biashara wa Zanzibar, Balozi Amina Salum Ali, amesema vijana wanapaswa kujiwekeza katika elimu ili waweze kunufaika na ajira katika sekta ya utalii na mabadiliko ya sayansi na teknolojia katika kuelekea uchumi wa kati wa viwanda Zanzibar.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Amina Salum Ali akizungumza na wanafunzi katika hafla ya uzinduzi wa vibaraza vya kusomea wanafunzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Zanzibar, vilivyojengwa na mradi wa Best Of Zanzibar, Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja mwishoni mwa wiki. PICHA: RAHMA SULEIMAN

Balozi Amina alisema hayo alipokuwa akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa vibaraza vya kusomea vilivyojengwa katika Chuo cha Utumishi wa Umma na kufadhiliwa na Kampuni ya Pannroyal Limited eneo la Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja.

“Sekta ya utalii Zanzibar kubwa na ndiyo yenye uwezekano wa kuinua uchumi wa Zanzibar kutokana na kuchangia pato la taifa asilimia 27 na fedha za kigeni aslimia 75 kwa mwaka,” alisema Balozi Amina.

Alisema Zanzibar ipo katika kipindi cha mpito cha kuelekea katika uchumi wa viwanda na kuimarisha sekta ya uwekezaji, hivyo lazima vijana wajiwekeze katika elimu ili waweze kunufaika na ajira katika sekta binafsi.

Alisema utalii ndiyo nguzo ya uchumi wa Zanzibar baada ya kuchukua nafasi ya zao la karafuu, ndiyo maana serikali imeamua kuimarisha miundombinu ya usafiri wa anga na barabara pamoja na sekta ya viwanda Visiwani Zanzibar

“Serikali imejipanga, lakini inabidi tujipange zaidi kwa sababu utalii unagusa mambo mengi ikiwamo miundombinu, huduma bora na lazima tuwe na vivutio vingi ili watalii waje na baadae warudi tena,” alisema.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Pannroyal Limited, Saleh Mohamed Said, alisema wakati umefika kwa serikali kusikiliza matatizo yanayowakabili wawekezaji katika sekta ya utalii Zanzibar.

Alisema watalii wanaotembelea Zanzibar wamekuwa wakipata usumbufu wanapofika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume kutokana na mfumo mbovu wa ukaguzi wa visa na chanjo katika sehemu wanazotoka na kulazimika kuchukua zaidi ya saa moja na wengine kudaiwa rushwa.

Alisema serikali lazima ichukue hatua za kuondoa matatizo ya rushwa wanayokutana nayo watalii pamoja na kero ya watembeza watalii wasio rasmi maarufu kama “papasi” katika maeneo ya ufukwe wa Zanzibar.

Aidha, alisema wakati umefika kwa Zanzibar kuanzisha kituo cha uwekezaji Zanzibar (One Stop Center) ili kuondoa tatizo la urasimu unaofanywa na baadhi ya viongozi na watendaji katika miradi ya vitenga uchumi.

000000