EPZA, Jiji Dar kupitia maeneo maalum ya uzalishaji

28Sep 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
EPZA, Jiji Dar kupitia maeneo maalum ya uzalishaji

MAMLAKA ya Maeneo Maalum ya Uzalishaji wa Mauzo ya Nje (EPZA), kwa kushirikiana na Mkoa wa Dar es Salaam wamefikia muafaka wa kupitia kwa pamoja maeneo maalum ambayo yatasaidia kusukuma mbele uchumi wa viwanda.

Akiongea wakati wa kufunga mafunzo maalum ya siku moja kwa maofisa wa serikali wanaounda kamati za uchumi na biashara kutoka katika halmashauri za jiji la Dar es Salaam, Katibu Tawala wa Mkoa, Paulo Makanza,  alisema kuwa kuna umuhimu wa kuanzishwa maeneo mengi ya viwanda ili kuchangia kusukuma uchumi wa viwanda nchini.

“Tukiendeleza maeneo mengi maalum ya viwanda itasaidia sana kuongeza ajira, mauzo ya nje na kuingizia nchi fedha za kigeni, pamoja na kukuza kwa kasi uchumi wa viwanda,” alisema.

Aliwataka wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na Watanzania kwa ujumla kutumia fursa hiyo ya kuwapo kwa EPZA na maeneo mbalimbali ya viwanda kujua kwa kina uwekezaji uliofanyika katika sekta ya viwanda nchini na manufaa ambayo yamepatikana hadi sasa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mipango na Maendeleo wa EPZA, Lamau Mpolo, alisema katika malengo ya muda mfupi, mafunzo hayo yatasaidia  kuboresha utoaji huduma kwa wawekezaji waliopo na wale wanatarajiwa kuja ikiwa ni matunda ya kufanyika kwa mafunzo kwa maofisa kutoka halmashauri za jiji hilo.

“Kupitia mafunzo haya tunaamini wawekezaji wanaopitia mamlaka ya EPZA na wale wanaopitia taasisi nyingine za serikali watapata huduma bora zaidi na kwa wakati,” alisema.

Katika malengo ya muda mrefu, alisema EPZA na Jiji la Dar es Salaam wanatarajia kuanzisha maeneo maalum ya uwekezaji bila kujali tofauti ya majukumu ya kila taasisi, lakini wote wakiwa na lengo la kuendeleza maslahi ya serikali kujenga uchumi imara wa viwanda.

Alisema lengo la mafunzo hayo ni kujenga uelewa wa pamoja kati ya taasisi hizo mbili na kuangalia kwa namna gani kila moja inaweza kutoa mchango mkubwa katika uendelezaji wa viwanda nchini.

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa anayeshughulikia uzalishaji na uchumi, Dk. Elizabeth Mshote, alisema mafunzo hayo yamewajengea uwezo na uelewa wa masuala mbalimbali yanayohusu uendelezaji wa viwanda nchini.

“Tumejifunza kwa vitendo kutoka katika mamlaka ya EPZA juu ya majukumu yao na namna ambavyo wanaweza kusaidia katika uanzishaji na ujenzi wa viwanda katika halmashauri zetu za Jiji la Dar es Salaam,” alisema.

Habari Kubwa