EWURA: Hakuna tatizo la petroli

01Jul 2020
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
EWURA: Hakuna tatizo la petroli

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imewahakikishia wateja wa mafuta ya petroli kuwa kuna lita 92,435,539 kwenye maghala zitakazotosheleza matumizi kwa siku 25.

Pia kuna lita 147,398,593 za dizeli zitakazotosheleza matumizi kwa siku 29 na taarifa za kuwapo kwa uhaba wa mafuta hayo mamlaka inazifuatilia kupitia wakaguzi wake wa mikoa na wilaya.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa EWURA, Mhandisi Godfrey Chibulunje, alisema hakuna tatizo la mafuta nchini.

Pia alisema maghala hayo ya mafuta yana lita 98,077,624 za petroli na lita 147,404,384 za dizeli kwa ajili ya soko la nje.

Chibulunje aliwataka wananchi kununua mafuta kwa bei elekezi iliyotolewa na serikali.

Alisema tayari kampuni 22 zina hifadhi ya mafuta ya petroli katika Bandari ya Dar es Salaam na kampuni 27 zina hifadhi ya mafuta ya dizeli.

“Katika maeneo yaliyotambulika kuwa na uhaba wa mafuta mamlaka ilielekeza vituo vya mafuta kununua petroli na dizeli kutoka kampuni mbalimbali ikiwamo Moil, Total, Oryx, Star Oil na Olympic Petroleum,” alisema.

Alisema hadi Juni 27, EWURA iliwezesha mafuta kufikishwa au kupakiwa katika maghala kuelekea maeneo yenye uhaba ambayo ni Chato, Chunya, Geita, Ifakara, Ngara, Sirari, Kasulu, Tabora, Nkasi na Vwawa.

“Juni 29, mafuta mengine yanatarajiwa kwa ajili ya kuelekea Geita, Biharamulo, Kibondo, Ilula, Iramba, Igunga, Kondoa, Kibaigwa, Mpwapwa, Kibondo, Kongwa, Mbande, Mvumi, Mlali, Manyoni na Kyela,” alisema.

Chibulunje alisema shehena ya petroli yenye tani 39,772 inategemewa kuwasili nchini Julai Mosi.

Habari Kubwa