Exim yachangia ununuzi vitanda vya wanafunzi

14Feb 2020
Na Mwandishi Wetu
Arusha
Nipashe
Exim yachangia ununuzi vitanda vya wanafunzi

BENKI ya Exim Tanzania imechangia kiasi cha Sh. milioni 25 kwa ajili ya ununuzi wa vitanda pacha 47 vya hosteli ya wanafunzi wa Shule mpya ya Sekondari ya Mrisho Gambo iliyopo mkoani Arusha.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Exim Tanzania, Jaffari Matundu (wa tatu kulia), akikabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya Sh. milioni 25 kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo (wa tatu kushoto), kwa ajili ya ununuzi wa vitanda pacha 47 vya hosteli ya wanafunzi wa Shule mpya ya Sekondari ya Mrisho Gambo. Wengine ni maofisa waandamizi wa mkoani humo na benki hiyo. MPIGAPICHA WETU

Hatua hiyo ni mwendelezo wa benki hiyo katika kuunga mkono jitihada za serikali katika kuboresha sekta ya elimu hapa nchini.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi msaada huo iliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Exim Tanzania, Jaffari Matundu alisema, mchango huo ni sehemu ya mpango wa uwajibikaji kwa jamii unaotekelezwa na benki hiyo ukifahamika kwa jina "Exim Cares" ukilenga kusaidia jamii.

"Benki ya Exim tunaamini kuwa tunalo jukumu kubwa la kufanya katika kuwezesha mabadiliko chanya katika jamii zinazotuzunguka. Elimu ni kati ya maeneo yetu ya kuzingatia na mpango huu unaendana na mkakati wetu wa kubadilisha maisha ya wanafunzi chini ya mpango wa 'Exim Cares' kupitia vitendo endelevu,” alisema.

Matundu alisisitiza kwamba: "Benki ya Exim tunavutiwa zaidi katika kuleta athari chanya kwenye jamii ambazo tunatoa huduma zetu, hivyo kwa kuangalia nafasi yetu tumeaona kwamba kwenye hili tunaweza kusaidia vitanda pacha vipatavyo 47 vikiwa na uwezo wa kubeba wanafunzi zaidi ya 100.”

Alitoa wito kwa taasisi na wadau nchini kuhakikisha wanawekeza kwenye uwezeshaji wa vijana kupitia elimu kutokana na ukweli kuwa bado wanakabiliwa na changamoto nyingi.

"Tumebaini kuwa kuna changamoto zinazoathiri vijana wa leo hususani wanafunzi ambazo zinaweza kuwaongoza kuelekea kwenye tabia zisizokubalika ndani ya jamii. Benki ya Exim, tunaamini kwamba kuna haja ya kuelekeza umakini na kuzingatia uwezeshaji wa vijana kupitia elimu. Tutaendelea kuwekeza katika hili na kutimiza wajibu wetu kwa miaka mingi ijayo,” aliahidi.

Alipongeza serikali kwa kutoa elimu ya msingi bure kwa watoto wote hatua ambayo imekuwa ni msaada mkubwa kwa watoto wanaopitia changamoto mbalimbali za kiuchumi ikiwamo yatima, watoto wenye mahitaji maalum ya kielimu pamoja na vikundi vingine vyenye vya watoto wanaoishi mazingira magumu.

Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, Gambo aliipongeza benki hiyo lwa msaada huo huku akibainisha kuwa umetolewa kwa wakati muafaka.

"Kupitia msaada huu kutoka benki ya Exim tutaweza kuwasaidia wanafunzi wetu kukaa hosteli, haswa wale ambao kwa sasa wanatembea umbali mrefu kwenda na kurudi. Kwa kweli kupitia msaada huu msaada huu utawawezesha kujifunza vizuri na kutambua ndoto zao za masomo, '' alisema Gambo.

Alisema mahitaji ya mradi huo ni vitanda 100 na magodoro ambayo utagharimu Sh. milioni 53.7.

Habari Kubwa